MAAMBUKIZI YA UKIMWI YAPUNGUA MGODI WA GGM
- Khalidi
- Dec 20, 2017
- 1 min read

Jitiada za Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Geita (GGM) kuazisha zoezi maalumu la kuhamasisha wafanyakazi wake kujitokeza kupima virusi vya ukimwi limefanikiwa kupunguza maambukizi kutoka asilimia 3.5 hadi 0.9 kati ya mwaka 2007 na 2016.
Daktari Mkuu wa GGM, Mtemi Rusasa, alisema upimaji huo ulianzishwa rasmi mwaka 2004 na umekuwa na mafanikio kila mwaka, kutokana na kupungua maambukizi mapya.
“Kwa mwaka huu tumeanza kupima wafanyakazi na familia zao tangu Desemba Mosi na zoezi litachukua wiki mbili na litakamilika Desemba 18, mwamko wa wafanyakazi kuja kupima ni mkubwa , alisema. Alishauri mashirika mbalimbali na taasisi za serikali kuzingatia sera ya Ukimwi mahali pa kazi kwa kujenga utamaduni huo ili kuondokana kupunguza na ikiwezekana kumaliza kabisa tatizo la maambukizi mapya miongoni mwa wafanyakazi.
DK. Rusasa, alisema GGM imekuwa ikishirikiana na Halmashauri za Wilaya na Mji wa Geita kufanya zoezi la kuhudumia walioambukizwa virusi ambao hupata dawa na ushauri nasaha.
“Kupitia ushirikiano huo, kila mwezi huwa tunafanikiwa kupima wastani wa wananchi 300 kila mwenzi , hivyo mwamuko wa wananchi kujitokeza kupima afya zao ni mzuri,” alisema.
Kwa upande wa magonjwa ya saratani ya shingo ya kizazi na vivimbe vya matiti, DK. Rusasa alisema wananchi mkoani humo bado wanamwamko mdogo kupima na wengine kujitokeza kupima wakiwa na hali mbaya.
Mmoja wa wafanyakazi wa Mgodi huo, kitengo cha Jiolojia aambaye alifikia katika Zahanati ya GGM kupima Afya, Amos Manoni, alisema zoezi hilo ni muhimu sana, na husaidia na kuwakumbusha wafanyakazi kuwa makini na afya zao.
Comments