ONYO WATUMISHI WASIO WAAMINIFU.
- Khalidi
- Dec 13, 2017
- 1 min read

Waziri wa Ulinzi na jeshi la kujenga Taifa (JKT), dk, Hussein Mwinyi, amesema wizara yake itaendelea kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watumishi wasio waaminifu.
Waziri Mwinyi alisema hayo alipokuwa akihutubia baraza la wafanyakazi la Wizara ya Ulinzi na JKT mjini Morogoro.
“Sitaogopa kumchukulia hatua za kinidhamu mtumishi katika utumishi wake,” alisema DK. Mwinyi.
Akisisitiza baraza kama wawakilishi wa watumishi wawasaidie wale wote wanaokwenda kinyume cha taratibu za kiutumishi kabla hawajachukuliwa hatua za kinidhamu.
Aidha, aliwataka watumishi wa wizara hiyo kufanya kazi na kuongeza ufanisi na utendaji katika kazi ili kuendana na kasi ya serikali ya Rais John Magufuli.
Pia alilitaka baraza kujadili kwa makini mpango wa Bajeti ya mwaka 2017/18 na 2018/19 na kutafuta majibu sahihi ya changamoto zilizojitokeza.
Akizungumzia ajira, Waziri Mwinyi alisema Wizara imepewa kibali na serikali cha kuajiri watumishi wanne ambao wameshaanza kazi.
Kuhusu kuhamia Dododma, Mwinyi alisema wizara inakamilisha taratibu za kuhamisha watumishi awamu ya pili wapatao 85 ambao wametarajiwa kuhamia mwishoni mwa mwezi huu.
Baraza lilijadili mambo kadhaa yakiwamo maboresho ya mahitaji mbalimbali ya watumishi, mpango mkakati wa kuboresha Shirika la Nyumba lililopo Kibaha mkoani pwani.
Comments