top of page

DK. KALEMANI AWAONYA MAKANDARASI WA REA

  • Khalidi
  • Dec 15, 2017
  • 1 min read

Waziri wa Nishati, DK. Medard Kalemani, amewaonya makandarasi wanaotekeleza mradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), wafanye kazi kulingana na mkataba uliopo.

Pia amewataka makandarasi hao wajenge miundombinu katika vijiji vyote vinavyopitiwa na mradi huo, ili kuwapa moyo wa kupata umeme wananchi walioko katika vijiji hivyo.

DK. Kalemani alitoa kauli hiyo juzi, katika Kijiji cha Milamba, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, alipokuwa akikagua miradi ya umeme.

“Makandarasi wanatakiwa kuwa makini kwa ujenzi wa mradi huo na wahakikishe hakuna mapungufu yoyote yanayoweza kujitokeza.

“Mradi huo unapaswa kuwafikia wananchi wote bila kuwapo na ubaguzi wa aina yoyte ili kutimiza malengo ya Serikali ya kufikisha umeme kwa kila mwananchi vijijini.

“Kwa hiyo, naagiza kwamba, mkandarasi atakayechelewa kumaliza mradi atakatwa asilimia 10 ya sehemu ya malipo yake kama sheria inavyosema.

“Nasema hivyo kwa sababu lazima tufuate sheria na hatuwezi kuwalinda wakati wanachelewesha umeme kwa wananchi vijijii,” alisema DK. Kalemani. Katika hatua nyingine, waziri huyo aliwataka watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuhakikisha wanafika kwenye vijiji vyote vinavyopitiwa na mradi wa REA, ili kuwaandikisha wananchi na kuchukua malipo ili wawaunganishie umeme haraka iwezekanavyo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota (CCM), alisema Tanesco wanapaswa kufanya matengenezo ya miundombinu kutokana na uchakavu uliopo katika miundombinu yao.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page