MABALOZI UGHAIBUNI WAKALIA KUTI KAVU
- Fahari News
- May 11, 2018
- 1 min read

Rais John Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na mabalozi kushindwa kutekeleza maagizo aliyowapa na kusema balozi atakayeshindwa kuonyesha ufanisi atarudishwa nyumbani ili kazi hiyo wapangiwe watu wenye uwezo.
Aliyasema hayo Ikulu Dar es salaam wakati wa hafla ya kuwapisha, Alphayo Kidata kuwa Balozi wa Canada na msalika Makungu kuwa katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora. Balozi Kidata pia ataiwakilisha nchi ya Cuba akichukua nafasi iliyoachwa na Balozi Jack Zoka ambaye amemaliza muda wake.
Makungu anachukua nafasi iliyoachwa wazi na DK. Thea Ntara ambaye amestaafu. Rais magufuli alisema alitoa maagizo mabalozi wote wampe taarifa juu ya utendaji kazi na manufaa ambayo nchi imeyapata kwa uwepo wa kila Balozi katika nchi aliyopangiwa kila robo mwaka, lakini hawafanyi hivyo.
“Nataka nijue katika kipindi ambacho Balozi ameteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchi Fulani, tumenufaikaje na uwepo wake kwenye nchi ile,” alisema Rais Magufuli na kueleza zaidi.
“Kuteuliwa sawa, lakini siyo lazima ukae katika ubalozi huo kwa kipindi chote ulichopangiwa “Ukishindwa kuleta manufaa unarudishwa na huko unapangiwa mtu mwingine atayeleta manufaa kwa nchi.”rais Magufulia alitaka Mabalozi kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kwa manufaa ya taifa na kutoa taarifa ya wanachofanya.
Comments