top of page

MADIWANI WACHAPANA MAKONDE KIKAONI

  • Fahari News
  • May 10, 2018
  • 2 min read

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mdeme amesimamisha kufanyika kwa kikao cha Baraza la Madiwani la Manispaa ya Songea, baada ya madiwani hao kuchapana makonde wakati wakiwa katika kikao cha kazi cha Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kikao hicho kitafanyika pale atakaporejea kutoka kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika wilaya ya Tunduru mkoani humo.

Kikao hicho cha Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo kilipangwa kufanyika jana, lakini kiliahirishwa baada ya madiwani hao kuchapana makonde wakati wakiwa katika kikao hicho kazi cha CCM juzi.

Kikao hicho kilikuwa kikiongozwa na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Songea Mjini, Juma Mpeli ambacho kilifanyika siku moja kabla ya kikao hicho. Uchunguzi uliofanywa mwandishi wa habari hizi ulibaini kuwa kikao hicho cha kazi kiliwahusisha madiwani wa CCM kwa lengo la ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya ilani ya chama hicho, kabla ya kufanyika kwa kikao hicho cha baraza cha robo ya tatu ya mwaka.

Uchunguzi huo ulibaini zaidi kuwa madiwani hao walianza kurushiana makonde baada ya kupishana kwa kauli kila upande ukimtuhumu mwenzake kuendesha ufisadi ndani ya Manispaa hiyo kutokana na madiwani hao kuwa wamegawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni lile linaloongozwa na Meya wa Manispaa hiyo,

Abdul Shaweji ambaye ni diwani wa kata ya Subira na la pili ambalo linaloongozwa na Naibu Meya, Yobo Mapunda, ambaye ni diwani wa kata ya Lilambo.

Diwani wa Kata ya Lizaboni katika Manispaa hiyo ya Songea, George Mbunda akihojiwa na gazeti hili aliutupia lawama uongozi wa CCM katika wilaya hiyo kwa kushindwa kuwaunganisha madiwani na kusababisha makundi hayo aliyosema yanachelewesha maendeleo.

Alisema Mkuu wa Mkoa Mdeme yupo sahihi kwa hatua yake aliyochukua ya kusimamisha kikao hicho, vinginevyo ingekuwa aibu kwa wananchi ambao wangefika kusikiliza mkutano huo wa madiwani.

Diwani huyo alisema hata baadhi ya wakuu wa idara na madiwani hawaelewani kitu ambacho ni hatari kwa mustakabali wa maendeleo ya Manispaa hiyo. Mkurugenzi wa Manispaa hiyo ya Songea, Tina Sekambo alipohojiwa alikiri kupokea barua kutoka kwa Mkuu wa Mkoa Mdeme ya kusimamisha kikao hicho cha baraza hilo la madiwani jana.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page