Milioni 14 wapata vitambulisho vya taifa
- Fahari News
- May 4, 2018
- 2 min read

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesajili wananchi 14,048,493, wageni 13,254 na wakimbizi 6,289 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Vile vile Idara ya Uhamiaji itaendelea na ufungaji wa mfumo wa hati za kusafiria za kielektoniki katika mikoa yote nchini.
Akiwalisha Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bungeni jana, Waziri wa wizara hiyo, Dk Mwigulu Nchemba alisema, utambuzi, usajili na utoaji wa vitambulisho vya Taifa ni wa kuishia Machi, mwaka huu.
Alisema usajili huo unakwenda sambamba na uchukuaji picha na alama za kibaiolojia ambao unafanyika katika mikoa yote ili kutengeneza vitambulisho bora na kuviwagawa kwa walengwa.
Dk Mwigulu alisema Mamlaka hiyo imeunganisha mfumo wake wa utambuzi na taasisi nyingine 35 ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa jamii na kuboresha hali ya ulinzi na usalama nchini.
“Aidha, Mamlaka imekamilisha ujenzi wa kituo cha kutunza kumbukumbu Kibaha, mkoani Pwani na Kituo cha Uokozi wakati wa majanga Kihonda, Morogoro pamoja na ofisi za usajili 13 katika wilaya mbalambali Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema.
Vile vile, Nida imeweka mtandao wa mawasiliano kati ya makao makuu na ofisi 117 za usajili za wilaya ili kusaidia kusafirisha taarifa kutoka wilayani kwenda kituo kikuu cha kutengeneza vitambulisho na kutunza taarifa.
Kuhusu hati za kusafiria za kielektoniki, Waziri Mwigulu alisema itaendelea kufunga mfumo wa visa za kielektoroniki na kufunga mifumo ya kudhibiti watu wanaongia na kutoka nchini. “Pia itaendelea kuweka miundombinu ya uwekezaji wa mtandao wa mawasiliano wa mifumo katika ofisi na vituo vya uhamiaji vya mipakani.”
Alisema hati hizo za kusafiria zinamwezesha mtumiaji kuwa na nakala yake ya hati kwenye simu yake ya kiganjani baada ya kupakua ‘App’ ya hati yake kwenye simu yake.
Kuhusu ulinzi na usalama mipakani, Waziri Mwigulu alisema, jumla ya wageni 1,021,071 waliingia nchini kuanzia Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu, ukilinganisha na wageni 1,032,978 waliongia katika kipindi kilichopita.
Katika kipindi hicho, jumla ya wahamiaji haramu 13,393 walikamatwa na kuchukulia hatua mbalimbali za kisheria, tofauti na wahamiaji 9,581 waliongia nchini mwaka uliotangulia, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 40 la wahamiaji hao.
Vile vile katika kipindi hicho Watanzania 211 waliokwenda nje ya nchi kinyume na taratibu za uhamiaji, walirudishwa nchini na wizara kupitia idara ya uhamiaji wataendelea kufanya misako na doria ili kubaini na kuwaondoa wahamiaji haramu.
Kuhusu jeshi la uokoaji, alisema katika kipindi hicho, jeshi hilo lilifanya ukaguzi katika maeneo 60,366 sawa na asilimia 74 ya lengo la kukagua katika kipindi hicho, na mkakati wake ni kuendelea kufanya ukaguzi katika maeneo mengi zaidi.
Alisema katika kipindi hicho, Jeshi la Magereza lilihifadhi wafungwa na mahabusu 39,763, kati yao wafungwa ni 20,312 na mahabusu 19,451 ulikinganisha na uwezo wa kuhifadhi wafungwa na mahabusu 29,902 ambapo ongezeko hilo ni sawa na asilimia 33.
Dk Mwigulu alisema katika kupunguza msongamano gerezani wizara inasimamia utekelezaji wa Programu ya Adhabu Mbadala wa Kifungo Gerezani ili kupunguza gharama za kuhudumia wafungwa na mahabusu.
Comments