MAREHEMU 12 WABADILI ADHABU KWA MADEREVA.
- Fahari News
- Apr 6, 2018
- 1 min read

Roho za marehemu 12 waliofariki kwa ajali ya barabarani juzi usiku zimeifanya serikali kuagiza dereva atakayekamatwa kwa kosa la kuendesha kwa mwendokasi apelekwe mahabusu na kisha mahakamani, kuanzia jana, kuanzia jana.
Agizo hilo lilitolewa Bungeni mjini hapa Mwigulu Nchemba, alipokuwa akitoa taarifa kuhusu ajali iliyohusisha basin a lori mkoani Tabora juzi usiku na kusababisha vifo vya watu 12 na majeruhi 46.
Aidha Rais John Magufuli amelitaka jeshi la polisi, na kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya kujitathimini na kutafuta majawabu ya ajali.
Ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Makomero wilayani Igunga baada ya basi la City Boys la kutoka Karagwe mkoani Kagera kwenda Dar es salaam kugongana na lori aina ya Mistubish Fuso lililokuwa linatoka Singida kwenda Igunga.
Katika taarifa yake, waziri Mwigulu aliagiza jeshi la polisi kuhakikisha linawakamata na kumpiga faini dereva yeyote atakayeonekana anaendesha gari kwa mwendo kasi na asiachwe hadi atakapofikishwa mahakamani.
Alisema mahakama ikijiridhisha kuwa ni kawaida ya dereva huyo kuendesha kwa mwendokasi, dereva husika anyang’anywe leseni.
“Pia nasisitiza kila basi la abilia liwe na madereva wawili ili mmoja akikamatwa mwingine aendelee na safari,” alisema Mwigulu.
Waziri huyo alilazimika kutoa kauli ya serikali bungeni baada ya mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga, aliyekuwa anaongoza kikao cha mchana, kuitaka serikali itoe ufafanuzi kuhusu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Ulanga Mashariki Goodluck Mlinga kuhusu ajali hiyo.
Mbunge huyo wa CCM alidai ajali hiyo imetokana na ubovu wa barabara na kuitaka serikali iwe inatoza faini kwa wakala wa Barabara (Tanroads) pale ajali zinaposababishwa na ubovu wa miundombinu kama ambavyo jeshi la polisi linafanya kwa madereva wanaobainika kufanya uzembe barabarani.
Comments