YONDAN, TSHISHIMBI, CHIRWA NA MAKAPU HAWATACHEZA DHIDI YA WA ETHIOPIA - CAF
- khalidi
- Apr 5, 2018
- 1 min read

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeitumia barua ya tahadhari Yanga kutowatumia wachezaji wake wanne, mabeki Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, kiungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi na mshambuliaji Mzambia Obey Chirwa katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Welaita Ditcha ya Ethiopia. Yanga watakuwa wenyeji wa Waleita Ditcha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Barua iliyoandikwa jana kutoka makao makuu ya shirikisho, Cairo nchini Misri imesema wanne hao pamoja na wachezaji wawili wa Welaita Ditcha, Teklu Tefesse Kumma na Eshetu Mena Medelecho hawaruhusiwi kucheza mechi hiyo baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano kila mmoja katika mechi zilizopita za timu zao.
Meneja wa Yanga, Hadidh Saleh amekiri kupokea barua hiyo na kuongeza kuwa "ni kweli wanafahamu Makapu, Tshishimbi na Chirwa wana kadi mbili za njano, lakini kwa Yondan kumbukumbu zao zinaonyesha ana kadi moja tu, tunajaribu kuwasiliana na CAF kupata ufafanuzi, maana sisi kumbukumbu zetu zinaonyesha ana kadi moja tu,”amesema Saleh.
Yanga imeweka kambi mjini Morogoro tangu juzi kujiandaa na mchezo huo
Comments