WANANCHI WATOA SIKU 90 MAGEREZA KUACHIA ENEO
- Fahari News
- Apr 3, 2018
- 2 min read

Mrogoro. Wakazi zaidi ya 3000 wa kijiji cha Mbigiri wilayani Kilosa wametoa notisi ya siku 90 ya kuitaka magereza kuachia eneo la eka zaidi ya 8,000 wanalodai limechukuliwa na jeshi hilo bila ridhaa yao.
Hata hivyo, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro, Mzee Ramadhani Nyamka alisema gereza hilo halijapora eneo lolote kwa wananchi bali kilichofanyika ni kurejesha maeneo ambayo wakulima walizoea kuyatumia.
“Ninavyoelewa hakuna eneo tulilopola maana hata miaka ya nyuma wananchi hawa walizoea kuandika barua kuomba kulima eneo lile wakati wa msimu wa kilimo na msimu unapopita huyarejesha,” alisema Nyamka.
Alisema magereza wanamiliki eneo la Mbigiri kihalali na tayari wana hati miliki inayotolewa mwaka 2017.
Awali, wakizungumzia hatua hiyo wakazi hao walisema eneo hilo walikuwa wakilitumia kwa kilimo cha mpunga kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita.
Walisema mwaka huu walipofika katika eneo hilo walishangaa kukuta likilindwa na askari huku wakiwazuia kuingia kwa maelezo kuwa ni mali ya Magereza.
Akizungumzia suala hilo, katibu wa wakulima hao Lunjino Peter alisema kwamba mgogoro huo ulianza tangu mwaka 1999.
Alisema jeshi hilo liliwapeleka wakulima mahakamani kwa madai ya uvamizi wa ardhi hiyo lakini wananchi walishinda kesi na kuruhusiwa kuendelea kulima katika eneo hilo.
“Katika kesi hiyo namba 203 ya mwaka 1999 tuliwashinda magereza na kupewa eneo letu kisheria, sasa mwaka 2016 mgogoro huu uliibuka upya wakati taasisi ya serikali zilipoagizwa kupima maeneo yake na ndipo Magereza walipochukua eneo la kijiji na kuhamishia kwao,” alisema Peter.
Alifafanua kuwa mwaka huu wakazi wa kijiji hicho wameshindwa kulima katika eneo hilo kutokana na ulinzi uliowekwa na magereza.
Akizungumzia notisi hiyo, mkulima John Kihelo alisema yeye na wenzake 3,000 wametoa notisi ya siku 90 kuazia Januari 29, 2018 kwa magereza kuachia eneo hilo.
Kihelo alisema kwamba iwapo magereza watashindwa kutekeleza wito huo wa kuwataka kuachia eneo hilo, watalazimika kuwapeleka mahakamani.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbigiri, Hemed Ibrahim alisema kitendo cha Magereza kuchukua eneo lao kinaathiri sana wananchi kwani hawana mahali pengine pa kulima.
Comentarios