WAZIRI SASA ATAKA WANAFUNZI WAPIGWE
- Fahari News
- Mar 26, 2018
- 2 min read

Waziri wa mambo ya ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amewataka waalimu kuendelea kutoa elimu bora kwa wanafunzi kwa kuwafundisha maadili mema na kwamba inapobidi matumizi ya fimbo yatumike.
Akizungumza katika harambee ya ujenzi wa mabweni ya shule ya sekondari Lulumba Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Waziri Nchemba alisema walimu wanatumia fimbo kunyoosha nidhamu za wanafunzi ili kutengeneza hatma ya nchi.
“Kunawakati waalimu wananyoosha nidhamu za wanafunzi lakini ninyi (wazazi) hamoni hii na kulalamika tu,” alisema waziri huyo.
“kinachofanyika (adhabu za viboko) ni kwa manufaa yetu…. Niwaombe (walimu) kwenye kutumia mifano tumieni mifano na kwenye kutumia fimbo fanyeni hivyo ili kutengeneza taswira ya nchi yetu.”
Adhabu ya viboko shuleni inaongozwa na sheria ya Elimu (sura 353), na hutolewa kwa ruhusa ya mwalimu mkuu tu na idadi ya juu ikiwa vine.
Aidha kanuni ya 3(1) ya sheria hiyo inasema adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima.
Hata hivyo, Waziri Nchemba alitaka walimu wote na si mwalimu Mkuu pekee kutumia fimbo hata katika adhabu zenye lengo la kunyoosha nidhamu za wanafunzi tu shuleni.
Wakati huo huo, waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi ametaka kuendelea kulindwa hadhi za walimu kwa kuwapatia miundombinu bora ya ofisi na vyumba vya madarasa.
Alisema majengo ya shule yanapaswa kuwa bora kulingana na maendeleo yaliyopo sasa nchini.
“Naunga mkono ujenzi huu wa mabweni ya wanafunzi, ukarabati wa vyumba vya madarasa na ofisi za walimu hivyo nachangia mifuko 200 ya saruji, nawaahidi pia kutoa sh. Milioni sita,” alisema katika hafla hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhaula alisema shule hiyo imekuwa ikifanya vinzuri kitaaluma kutokana na umahili wa walimu kwani watoto hao wanajua kujieleza kama vile wanasoma chuo kuku.
Alisema wakazi wa Iramba wanatakiwa kujivunia kuwa na shule zao pamoja na walimu hao ili kuboresha elimu wilayani humo.
“Unafanya jitihada ili kuhakikisha kila sekondari kunajengwa mabweni ili kuondoa kero za wanafunzi,” alisema Luhaula. “Sisi wa Iramba tulishindwa wenyewe kukutumia (Nchemba).”
“Nimekuwa mbunge lakini anayoyafanya mbunge huyu mimi sikuyafanya,” alisema Luhaula.
Comments