UPELELEZI WA KESI YA MKE MSUYA HAUJAKAMILIKA
- Fahari News
- Mar 15, 2018
- 1 min read

Upande wa Mashtaka katika kesi ya mauaji inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita (41), umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Wakili wa serikali, Elia Athanas alieleza hayo jana, mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati shauri hilo lilipotajwa.
Mbali na Mrita, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo namba 5 ya mwaka 2017 ni mfanyabiashara Revocatus Muyela (40) na wote wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji ya dada yake Erasto Msuya, Aneth Msuya.
“Mheshimiwa hakimu, licha ya upelelezi wa shauri hilo kutokamilika, jalada la kesi hii bado lipo mikononi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwaajili ya kulifanyia uamuzi,” alidai wakili Athanas. Februari 21 na Machi 6, mwaka huu upande wa mashtaka ulidai mahakamani hapo kuwa jalada la kesi hiyo lipo kwa DPP kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alikubaliana na upande wa mashtaka na kusema: “Nataka tarehe itakapotajwa, upande wa mashtaka mje na sababu za uhakika kwa nini kesi hii inachukua muda mrefu kukamilika kwa upelelezi.”
Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 19, mwaka huu, itakapotajwa. Washtakiwa wanadaiwa kumuua kwa makusudi Aneth Msuya katika tukio lililotokea Mei 25,2016, maeneo ya Kibada, Kigamboni jijini Dar es salaam.
Comments