SIRRO AELEKEZWA KAMATA KAMATA MAANDAMANO
- Fahari News
- Mar 12, 2018
- 1 min read

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba, amesema amemwagiza na kumwelekeza Mkuu wa Jeshi la polisi (IGP) Simon Sirro, kuwakamata watu wote ambao wamepanga njama za kutaka kuwaua watanzania katika maandamano ambayo wameyapanga kuyafanya.
Mwigulu aliyabainisha hayo jana alipokuwa akitoa salamu zake kwa Rais Magufuli aliyepo mkoani Singida katika ziara yake ya kikazi ambapo amezindua kiwanda cha alizeti na kusema anachotafuta katika maandamano hayo ni namna ya watu wanavyotawanywa tawanywa ili kusudi waje kulalamika kuwa serikali ndiyo imeua watu wake.
“Njama hiyo tumeiona na mimi nimemweleza IGP Sirro kwamba hata kupanga njama ya kuua ni kosa, wachukuliwe hatua kwa watu wanaopanga mipango ya aina hiyo na kuchafua taswira ya nchi yetu ama kwa mipango yao au wale wanaowatuma,” alisema na kuongeza:
Watu wanaotaka mikusanyiko ili wafyatue na kuua watu ili kchafua taswira ya nchi yetu na tunayo mifano ya maneno waliwahi kufanya jambo la aina hiyo na hatua zitachukuliwa,” alisema Mwigulu.
“Mheshimiwa Rais, ndiyo maana unaona vinyago vinyago vingi hivi kama hivi juzi alitokea kijana mdogo amesema ametekwa, eti ametekwa na akapata muda wa kutafuta pafyumu na nguo za kubadilisha kule atakakokuwa ametekwa. Unatoa wapi muda wa kujiandaa.
Watu wanatafuta njia ya kuharibu taswira ya nchi yetu, na jambo hili kama ambavyo ulishatoa maelekezo, si jambo ambalo tutacheza nalo wala mjadala, hakuna sababu ya maandamano wala hakuna sehemu ya kuandamania na hakuna ruhusa ya kuandamana.”
“Ikitokea hata watu wakaandamana ndani ya nyumba wakazunguka kitanda na akatokea mtu akaumia, Yule aliyeitisha waandamane pale atakuwa na lakuwajibika kwa sababu watu wanafanya mzaha na maisha ya dira ya nchi yetu ambapo rais amejitoa mhanga kwaajili ya kutengeneza urithi wa watoto wa Tanzania,” alisema Mwigulu.
Comments