top of page

HIKI NDO CHANZO CHA WANAWAKE KWENDA KWA WAGANGA WA KIENYEJI

  • Fahari News
  • Mar 9, 2018
  • 2 min read

Kilele cha siku ya Wanawake Duniani kilihitimishwa jana katika mikoa mbalimbali nchini kwa shughuli mbalimbali zilizoandaliwa na mashirika ya jamii ya Taifa na mataifa.

Katika maadhimisho hayo, makundi ya wanawake na baadhi ya wanaume waliopazwa sauti zao kuhusu masuala mtambuka yanayowakabili wanawake kwa njia moja ama nyingine.

Mshiriki kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria Kinondoni (Kipa), Anthony Isakwi alieleza kuwa vitendo vya ukatili wa jinsia ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuongeza idadi ya wanawake wanaokwenda kwa waganga wa jadi.

Akizungumza katika maadhimisho yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Isakwi alisema unyanyasaji wa jinsia unachangia wanawake wengi kutafuta mbinu mbadala za kudumu katika ndoa iliwamo kwenda kwa waganga wa jadi.

“Nimefanya kazi ya uganga wa jadi kwa zaidi ya miaka tisa, lakini zaidi ya asilimia 90 ya wateja wangu walikuwa wanawake,” alisema Isakwi.

Alisema chanzo cha yeye kuwa mganga ni baada ya baba yake mzazi kufariki dunia na mama yake kuingia kwenye manyanyaso kutoka upande wa baba yake waliomtaka arithiwe na mtoto wa shangazi yake, lakini alitaka na kuamua kuondoka bila kupewa chochote.

Alisema katika kipindi hicho waliishi maisha magumu, jambo ambalo limemfanya kuingia kwenye kazi ya uganga wa jadi bila kufahamu dawa halisi ni zipi.

Isakwi alisema katika kipindi hicho, wateja wake walikuwa wakihitaji dawa za kuimarisha mapenzi, kupata fedha kwa wapenzi, mimba na kuwaroga wake wenzao.

Alisema kwa kuwa alihitaji fedha aweze kumudu maisha alilazimika kujenga uhusiano wa Wamasai wa Kariakoo wamsaidie dawa hizo ambazo alizinunua.

Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo, Mbunge wa Viti Maalum (Kaskazini Unguja), Angelina Malembeka alisema kukosekana kwa sera inayomtetea mwanamke na mtoto kumechangia kukithiri vitendo vya unyanyasaji wa jinsia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga alishauri mila na desturi zilizopitwa na wakati ziachwe kukomesha manyanyaso, ukandamizaji na dhuluma kwa wanawake.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page