top of page

RPC AWA MBOGO BAMBIKA KESI

  • David
  • Mar 5, 2018
  • 2 min read

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa polisi, Ahmed Msangi amewataka askari kuepuka kubambikia kesi wananchi kwa kutaka rushwa na ubabaishaji. Badala yake, Kamanda Msangi ametaka askari mkoani mwake kufanya kazi kwa utii, nidhamu na maadili kama ambavyo sheria inaelekeza.

Kamanda huyo aliyasema hayo juzi alipokutana na askari wa wilaya ya Sengerema katika ukaguzi anaoendelea kuufanya katika wilaya na vikosi vyote mkoani Mwanza. Msangi aliwataka askari kukomesha vitendo vya ubambikaji kesi na kutolea mfano wa mashauri ya madai kubadilishwa kuwa kesi za jinai jambo ambalo linanyima haki wananchi na kuchafua sifa nzuri ya Jeshi la polisi.

Kamanda Msangi alisema askari yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake na kwamba kila askari atumie vinzuri dhamana aliyopewa na serikali na kulinda wananchi pamoja na mali zao. Alisema askari watafanikiwa kutimiza wajibu huo adhimu kwa kusimama vyema nafasi zao za utendaji.

“Askari muwe na utaratibu mzuri wa upokeaji, utunzaji na uondoshaji wa vielelezo katika vituo vya polisi,” alisema zaidi Kamanda Msangi na kufafanua. “Katika baadhi ya vituo lipo tatizo la utumzaji wa vielelezo… sitaki kuona tatizo linaendelea kuwapo, maofisa wa polisi wa wilaya kuzingatia taratibu zilizowekwa kisheria za uondoshaji wa vielelezo katika vituo vya polisi.”

Kwa upande wa upelelezi, Kamanda Msangi alisema kumekuwa na tatizo la ucheleweshaji katika kesi nyingi, jambo ambalo linawanyima wananchi haki. Alimtaka mkuu wa upelelezi wilayani hapo kushughulikia suala hilo mapema, ili haki ipatikane haraka bila uonevu wa aina yoyote.

“Ninawapongeza askari wa wilaya hii kwa utendaji mnzuri wa kudhibiti uhalifu,” juhudi kwa yale maeneo yenye vibaka na uhalifu mwingine mdogomdogo. Naamini mnaweza. “Ushirikiano ulipo na viongozi wa ulinzi na usalama wilaya, wananchi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama udumishwe, ili Sengerema iwe salama zaidi kwani amani ikiwepo maendeleo yatapatikana zaidi.”

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page