top of page

DK NCHEMBA : BODABODA ZINAZOSHIKILIWA POLISI ZIREJESHWEKWA WAHUSIKA

  • David
  • Mar 4, 2018
  • 2 min read

Arusha. Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba amewaagiza makamanda wa vikosi vya usalama barabarani kuwarudishia waendesha bobaboda pikipiki zao zilizokamatwa kwa makosa madogo ya barabarani.

Hata hivyo, ameagiza kuendelea kushikiliwa pikipiki zenye makosa makubwa yakiwamo ya dawa za kulevya, ujambazi wa kutumia silaha na utekaji.

Alitoa maagizo hayo jana alipozungumza kwenye mkutano wa umoja wa waendesha bodaboda jijini Arusha (Uboja) wakati alipowakabidhi pikipiki wanachama wa waliokopeshwa na kumaliza kuzilipia.

Katika miji kadhaa nchini ambako pikipiki hutumika kusafirisha abiria, kibiashara ya vyombo hivyo vya moto vimekuwa vikikamatwa na kupangwa kwenye vituo vya polisi.

Baadhi ya wamiliki wa pikipiki hizo wamekuwa wakiziacha kwa muda mrefu kutokana na kile kinachoelezwa ni kutokana na kukosa fedha za kulipia faini.

Mbali ya hilo, waziri Nchemba amewataka askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani kuacha kuwatoza faini madereva wa bodaboda kiwango sawa na wanachotozwa wale wa mabasi.

“Si haki kumtoza mwendesha bodaboda faini ya Sh30,000 kwa kosa la barabarani wakati ana abiria mmoja na kiwango hichohicho unamtoza dereva wa basi kubwa, hapa lazima tuangalie njia sahihi ya kushughulikia makosa haya,” alisema Dk Nchemba.

Kuhusu madereva wa bodaboda aliwataka kuheshimu kazi yao na kuona kusafirisha abiria kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni wajibu muhimu unaoweza kuwakwamua kiuchumi badala ya kujiingiza katika kusaidia uhalifu.

Dk Nchemba alisema iwapo waendesha pikipiki watajiheshimu na kuacha tabia ambazo hazifai katika jamii ambazo ni ukorofi wanaposimamishwa kwa kukiuka makosa ya barabarani, Kikosi cha Usalama Barabarani kitaacha ukamataji usio na heshima.

“Wakati mwingine unakuta polisi wanakimbizana na ninyi kwa sababu hamtaki kutii sheria, hii inasababisha madhara mengi yakiwamo ajali na wakati mwingine vifo, badilikeni na muone hii ni kazi ya heshima,” alisema.

Waziri huyo alisema Serikali inaandaa utaratibu wa kuwawezesha waendesha pikipiki kuanza kuwabeba watalii kutembelea mitaa ya majiji kadhaa nchini baada ya kuona waendesha pikipiki wa Arusha wanajiheshimu.

Dk Nchemba alisema utaratibu wa aina hiyo utaongeza mapato kwa kuwa na utalii wa ndani ya jiji badala ya ule wa kutegemea wanyamapori pekee.

Mwenyekiti wa Uboja, Maulid Makongoro alisema kupitia umoja wao, wamewadhibiti kimaadili wanachama ili wafanye kazi kwa kuzingatia miongozo waliyojiwekea.

Alisema hivi karibuni wataanza utaratibu wa kuvaa kikoti chenye namba na eneo analoegesha pikipiki dereva husika ili mteja akipatwa na tatizo iwe rahisi kumpata.

Alisema awali, umoja huo ulipata upinzani kutoka kwa wanasiasa waliouponda lakini kupitia ofisi ya mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa wameweza kusimamia maadili ya wanachama hadi kurejesha fedha walizokopeshwa pikipiki.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema waliwakopesha vijana 200 pikipiki zenye thamani ya Sh400 milioni na hadi sasa Sh355 milioni zimesharejeshwa na wahusika kukabidhiwa kadi kwa ajili ya umiliki rasmi.

Alisema Sh200 milioni zitakopeshwa kwa wanawake ili kuanzisha na kuendeleza shughuli za kujitafutia kipato na hasa ambao hawana namna ya kupata mikopo midogomidogo kutoka taasisi za fedha.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page