top of page

AJIRUSHA BAHARINI KINA KIREFU SAFARINI Z’BAR

  • David
  • Feb 28, 2018
  • 1 min read

Mwanaume mmoja ambaye jina lake bado halijafahamika amejirusha baharini kutoka katika boti ya Azam iliyokuwa ikitokea jijini Dar es salaam kuelekea Zanzibar Jumatatu, katika eneo linalohisiwa kuwa na kina kirefu.

Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii jana inaonyesha boti hiyo ikiwa imesimama eneo ambalo mwanaume huyo alijirusha huku watu wakijadiliana namna ya kumwokoa.

Tukio hilo limeelezwa kufanyika katika eneo la Bahari ya Hindi “ukishapita Msasani” ambako kuna mkondo wa maji unaodhaniwa kusababishwa na kina kirefu cha maji.

Eneo hilo lipo mwendo wa nusu saa kutoka Bandari ya Dar es salaam , kwa boti ziendazo kasi. Safari mpaka Zanzibar huchukua saa mbili.

Video hiyo inaonyesha abiria wakiwa wanashangaa uamuzi wa mtu huyo kujitosa baharini huku wengine wakisikika wakisema kuwa anaonekana akiogerea .

Baadhi ya waliokuwa kwenye Boti hiyo walisikika kwenye video hiyo wakiomba wapewe nafasi wajitose kwenda kumtafuta kwani wao ni mahiri kwenye uogeleaji.

“Kama vipi tumfuate wengine tunaweza (kuogelea)… anaonekana Yule kule tuacheni sisi tunaoweza kuogelea tukamchukue kwasababu tunaweza jamani,” alisikika mtu huyo akimuomba mmoja wa wahudumu wa boti hiyo huku akirekodi video.

Taarifa kutoka ndani ya Azam zilisema mabahalia wa boti hiyo walijitahidi kumtafuta mwanaume huyo eneo alipojitosa lakini hawakufanikiwa.

“Baada ya mwanaume huyo kujirusha baharini nahodha wa boti aliambiwa airudishe boti nyuma hadi eneo linalodhaniwa kuwa ndipo alipojitosa, lakini hawakufanikiwa (kumuona). Walirudi wenyewe tu,” alisema mmoja wa mashuhuda.

Aidha ,shuhuda huyo alisema baada ya kumkosa, walijadiliana kwa muda kuhusu nini kinaweza kufanyika na hatimaye waliona hawana namna zaidi ya kuendelea na safari ya Zanzibar.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, kamanda wa polisi wa mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo alisema waulizwe watu wa polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page