SERIKALI YAZITOZA FAINI YA MABILIONI MELI 19, YAELEZA SABABU
- David
- Feb 24, 2018
- 3 min read

Serikali imeziamuru meli 19 za uvuvi kulipa faini ya jumla ya Dola za Marekani 8,636, 363 sawa na Sh bilioni 19 ndani ya siku 14 baada ya kukiuka masharti ya leseni zao na kushiriki vitendo vya uvuvi haramu na uchafuzi mkubwa wa mazingira katika ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu.
Mbali na kutakiwa kulipa faini hizo, serikali pia imeiagiza Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) kuwaandikia notisi wahusika wa meli hizo kuwajulisha kuhusu maamuzi hayo na pia kuijulisha Kamisheni ya kusimamia samaki aina ya Jodari Bahari ya Hindi (IOTC) juu ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania kuhusu meli hizo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alisema jana mjini Zanzibar kuwa uamuzi huo wa serikali umekuja kutokana na meli hizo kukiuka Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 1998 Kanuni ya 10 ikisomwa kwa pamoja na Kanuni ya 68 ya Kanuni za Uvuvi wa Bahari Kuu za Mwaka 2009 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016. Mpina alisema zimekiukwa sheria hiyo kwa kutoripoti katika Bandari za Dar es Salaam, Zanzibar, Mtwara au Tanga kwa ajili ya ukaguzi kabla ya kuondoka katika Bahari Kuu ya Tanzania.
“Kwa kitendo hiki cha kukiuka masharti haya ya leseni zao maana yake wameshiriki uvuvi haramu, wamechafua mazingira kwa kiasi kikubwa wamefanya uvuvi holela na makosa mengine ya baharini vitendo hivi vimekuwa vilikosesha taifa mapato kwa kiasi kikubwa na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli haitakubali tena kuchezewa na kugeuzwa Tanzania kuwa shamba la bibi, kwa kila mmoja kuja na kuvua anavyotaka katika bahari yetu,” alisema Mpina.
Aliongeza kuwa serikali haiko tayari tena kufanya kazi na watu wanaovunja sheria za nchi na kwamba operesheni ya kuzisaka meli hizo itaendelea na zitaendelea kukamatwa kila siku kwani uhuru waliokuwa nao wa kuiba rasilimali hizo za taifa, haupo tena katika awamu ya tano. Alisema eneo la bahari lenye ukubwa wa kilometa za mraba 223,000 limekuwa likinufaisha mataifa mengine na kwamba msimamo wa serikali kwa sasa ni kuhakikisha rasilimali hizo zilizomo ndani ya eneo hilo zinachangia katika ukuaji wa Pato la Taifa.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Uvuvi, Dk Yohana Budeba alisema serikali imedhamiria kwa nguvu zote kulinda rasilimali za uvuvi na kudhibiti uvuvi haramu hivyo meli hizo zinazopewa leseni na kushindwa kufuata masharti zitaendelea kuchukuliwa hatua, na maagizo yote ya waziri atayasimamia ili yatekelezwe kwa wakati. “Serikali haina mchezo katika jambo hili itaendelea kuchukua hatua kali kwa lengo kulinda rasilimali hizi ili ziweze kunufaisha Watanzania na taifa kwa ujumla,”
alisema Dk Budeba.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa DSFA, Hosea Mbilinyi alizitaja meli hizo zinazotakiwa kulipa faini hiyo ambayo kila moja italipa Sh bilioni moja kuwa ni Tai Hong no.2, Tai Hong no. 8, Tai Xiang no.5, Tai Xiang no.5, Tai Xiang no. 8, Tai Xiang no. 9, Tai Xiang no. 9, Tai Xiang no. 10, Tai Xiang no.7, Tai Xiang no 6, Tai Hong no 6, Tai Hong no .7, Xian Shiji no. 81, Xin Shiji no. 82, Xin Shiji no. 83, Xin Shiji no. 86, Xin Shiji no.76, Xin Shiji no. 76, Jian Shen no.1 Wakili wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Divisheni ya Mashtaka Makao Makuu Dar es Salaam ambaye pia ni Mkuu wa Dawati la Makosa ya Mazingira na Maliasili, Wankyo Simon alisema wamiliki wa meli hizo wasipolipa fedha hizo ndani ya muda uliotolewa na serikali, taratibu za kuwafikisha mahakamani zitafanyika. Aidha, Wankyo alisema mbali na hatua hizo za mahakama, pia serikali itawasiliana na nchi zilizotoa bendera kwa meli hizo ili kuzifutia usajili na kutoruhusiwa tena kufanya shughuli za uvuvi katika sehemu yoyote duniani.
コメント