WATU 20 WAFA KWA KIPINDUPINDU DODOMA
- Fahari News
- Feb 21, 2018
- 1 min read

Jumla ya watu 20 wamefariki dunia mkoani Dodoma katika kipindi cha kuanzia Oktoba mwaka jana hadi Februari 19 mwaka huu, kutokana na ugonjwa wa kipindupindu huku watu 471 wakiugua ugonjwa huo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, DK. James Charles, mjini hapa huku ikielezwa kuwa Wilaya ya Mpwapwa inaongoza kwa vifo na wagonjwa wengine.
“Kuanzia Oktoba mwaka jana mkoa uliopata mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu ugonjwa huo ulianzia Wilaya ya Chamwino katika kijiji cha Mlowa na baadaye ulisambaa katika wilaya nyingine za mkoa wetu,” alisema DK. Charles.
Hata hivyo alisema ugonjwa huo ulithibitishwa lakini ilipofika Desemba mwaka jana, mlipuko huo uliongezeka kwa kasi katika Wilaya za Mpwapwa na Chamwino.
“Tangu kulipuka kwa ugonjwa huo hadi kufikia jana jumla ya watu 471 waliugua ugonjwa huo na miongoni mwao, 20 walifariki dunia” alisema.
Kwa mujibu wa DK Charles, Wilaya ya Mpwapwa ndiyo imetoa wagonjwa wengi zaidi takribani 322. Dk. Charles alisema sababu za Wilaya hiyo kuwa na wagonjwa wengi zaidi ni kutokana kuwapo uhaba mkubwa wa maji jambo ambalo ni kichocheo kikubwa cha ugonjwa huo.
Vilevile alitaja changamoto nyingine kuwa ni usafi wa mazingira, ulaji na maandalizi ya vyakula yasiyo salama katika maeneo ya biashara.
Katika kukabiliana na hali hiyo, DK Charles alisema mkoa umeongeza udhibiti na kutoa elimu ya afya kwa wananchi kuhusu kukabiliana na wagonjwa waliopo makambini wakiendelea na matibabu hadi jana walikuwa wamebakia 13.
Comentários