MWALIMU AUA MKE NA KUJINYONGA WAKIGOMBEA NYUMBA MOROGORO
- Fahari News
- Feb 20, 2018
- 1 min read

Morogoro. Mwalimu wa shule ya msingi Duthumi wilayani Morogoro, Respicius Salehe (46), amemuua mke wake, Scrinda Andrew (42) kwa kumjeruhi na kitu chenye ncha kali kichwani na baadaye nae kujiua kwa kujinyonga chanzo kikiwa ni ugomvi uliotokana na kuuza nyumba yao.
Akizungumzia tukio hilo kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Ulrich Matei alisema lilitokea Februari 17 mchana maeneo ya Lukobe.
Kamanda Matei alisema mwili wa mwalimu huyo ulikutwa ukining’inia kwenye mti wa mwembe baada ya kujinyonga kwa kutumia kitenge siku moja baada ya kumuua mkewe.
Alisema ugomvi uliosababisha mauaji ya wanandoa hao ulitokea baada ya mke kumpinga mumewe aliyetaka kuuza nyumba yao iliyopo Lukobe Manispaa ya Morogoro.
Hata hivyo, Kamanda Matei alisema polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kubaini sababu zaidi ya mauaji ya wanandoa hao na kwamba marehemu wote wameshazikwa.
Katika tukio jingine, Dominick Chilala aliuawa kwa kupigwa na risasi shingoni na mguuni ikielezwa kwamba ni wakati alipokuwa akijaribu kuiba Ng’ombe kwenye zizi.
Tukio hilo lilitokea Februari 15 mchana maeneo ya Makambarani. Ilielezwa kuwa mtu huyo aliuawa na Zephania Masawe baada ya kufyatua risasi kutoka kwenye bunduki aina ya shortgun mtu huyo alipoingia kwenye zizi lake.
Kamanda Matei alisema kabla ya kuuawa, mtu huyo alikuwa akitafutwa na jeshi la polisi kwa muda mrefu kwa tuhuma za kuhusika kwenye matukio ya wizi wa mifugo.
Comments