top of page

WAZIRI MKUU AAGIZA ZAHANATI IFUNGULIWE

  • khalidi
  • Feb 19, 2018
  • 1 min read

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Mganga mKuu wa Wilaya ya Magu, DK. Nindwa Maduhu, ahakikishe Zahanati ya Bugabu inafunguliwa.

Alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi na wananchi wa Wilaya ya Magu katika Kituo cha Afya cha Kahangara.

Waziri Mkuu alishangaa kuona zahanati imekamilika na inavifaa vyote vinavyotakiwa katika utoaji wa huduma, lakini watumishi hawajapelekwa ili wananchi wahudumiwe.

Alitoa agizo hilo baada ya wananchi kumwomba awasaidie kufunguliwa kwa zahanati ya kijiji chao ili waweze kupata huduma za afya karibu na makazi yao. Wananchi hao walidai kwa sasa wanalazimika kutembea umbali wa kilometa tisa kufuata huduma za afya katika kituo cha Afya cha Kihangara.

Kwa upande wake DK. Maduhu alisema tayari watumishi walishahamishiwa katika zahanati ya kijiji hicho na leo watakwenda na kuanza kuwahudumia wananchi.

Pia Waziri Mkuu amemtaka mganga huyo kuhakikisha dawa zinazonunuliwa wilayani humo ni zile zinazolingana na magonjwa yanayopatikana ndani ya maeneo yao.

Kabla ya kuzungumza na wananchi na watumishi, Waziri Mkuu alikagua na kuweka jiwe la msingi la uboreshaji wa kituo cha Afya Kahangara.

Mradi wa kuboresha kituo hicho chenye uwezo wa kuhudumia watu 26,321 ulianza Oktoba 30, 2017 na umegharimu Sh milioni 500.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page