Rais wa Fifa, CAF ndani ya Tanzania
- david
- Feb 19, 2018
- 2 min read

Kwa mara ya kwanza katika historia ya soka Tanzania, vigogo wa juu katika Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa na lile la Afrika, CAF watakuwa nchini kwa mkutano maalumu kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya soka.
Rais wa Fifa, Gianni Infantino atashiriki katika mkutano huo maalumu uliopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia keshokutwa.
Mkutano huo utashirikisha nchi wanachama 19 za Fifa, utafanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) unajulikana kwa jina la “Fifa Executive Football Summit” itawakilishwa na Rais na Katibu wake mkuu.
Tanzania ni nchi pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati iliyopewa heshima ya kuandaa mkutano huo ambao pia utajadili masuala ya soka la wanawake, vijana na mfumo wa usajili wa kielektroniki wa TMS ambao kwa sasa utakuwa chini ya Fifa wenyewe na si wakala.
Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi mkubwa wa Fifa kutembelea Tanzania na kubwa zaidi ni kupewa nafasi ya mkutano wa siku moja ambao viongozi wa mashirikisho ya soka katika nchi mbalimbali watashiriki.
Madhumuni hasa ya mkutano huo ni kuirejesha Fifa kwenye mpira wa miguu na mpira wa miguu kwa Fifa, kupanga mikakati ya maendeleo ya siku za usoni ikiwa ni pamoja na mataifa 12 duniani kupewa heshima ya kuandaa mikutano hiyo.
Mbali ya viongozi wa Fifa, pia viongozi wakuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) nao watakuwepo. “Hii ni heshima na tumepewa nafasi kutokana na utawala bora ambao kwa kipindi cha miezi mitano tangu tuingie madarakani tumeonyesha,” anasema Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Wallace Karia.
Anasema kuwa kwa kipindi kifupi, wamerejesha heshima ya TFF katika ramani ya soka katika Afrika na Duniani bila kusahau Ukanda wa Cecafa ambao juzi ilimchagua kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji. Miongoni mwa wajumbe 64 wanaoandamana na Infantino ni pamoja na makamu wake Mkuu, David Chung na viongozi wengine wakiwemo wa mabara, Salman Bin Ibrahim Al-Khalifa, Aleksander Ceferin, David Gill, Alejandro Dominguez, Victor Montagliani na Katibu Mkuu, Fatma Samoura.
Mataifa yatakayoshiriki mkutano huo ni Bahrain, Palestina, Saudi Arabia, United Arabs Emirates (UAE), Algeria, Burundi, Afrika ya Kati, Ivory Coast, Mali, Morocco, Niger, Tunisia, Bermuda, Monserrat, St. Lucia, Us Virgin, Maldives, Congo Brazzaville na wenyeji Tanzania.
Comments