top of page

FAMILIA ILIVYOPONA KUUNGUZWA KWA MOTO

  • Fahari News
  • Feb 19, 2018
  • 1 min read

Familia ya mkazi mmoja Mwangata Msikitini katika manispaa ya Iringa jana ilinusurika kuteketea kwa moto baada ya majirani kuwaokoa kwa kufumua dirisha la nyuma ya nyumba yao.

Tukio hilo limetokea majira ya saa 5:30 asubuhi wakati familia ya Onesmo Cosmas ikiwa ndani ikiendelea na shughuli. Chanzo cha moto kinadaiwa kuwa ni mtungi wa gesi kulipuka.

Wananchi wamekuwa wakihangaika kuzima moto kwa kutumia mipira ya maji, maji ya ndoo na mchanga ambapo iliwashinda na kuomba msaada kutoka Jeshi la Zimamoto.

Cosmas ambaye ameoa mzungu, hakuwepo wakati ajali hiyo ikitokea lakini alifika baada ya kupigiwa simu na mkewe. Mke wa Cosmas aligoma kuongea na vyombo vya habari vilivyofika kushuhudia tukio hilo la moto, wala kujitambulisha.

Majirani waliookoa familia ya Cosmas kwa kufumua dirisha la nyuma ya nyumba na kuanza kuitoa kupitia dirisha hilo, baada ya kushindwa kutokea mlangoni ambapo ilisadikika moto ulianzia.

Sehemu ya mbele kuna nyumba ya nyasi ambayo ilitumika kama sehemu ya kupumzikia wageni. Kamanda wa zima moto na Uokoaji Mkoa wa Iringa, Mrakibu Msaidizi JamesJohn alithibitisha kutokea kwa moto na kusema kuwa amefanikiwa kuzima kabla haujaleta madhara.

Alisema kuwa walipigiwa simu na wananchi majira ya saa 5:30 asubuhi na hatimaye kufanikiwa kuthibiti moto kabla haujasambaa katika nyumba za majirani.

Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zima moto huyu alisema nyumba iliyoungua haikuwa na umeme na chanzo cha moto bado hakijafahamika, ila unaonekana ulihama kutoka sehemu moja.

Aidha kamanda huyo waliomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi kwa kupiga simu ya dharura ambayo ni 114 bure na kuwaasa wasitumie namba hiyo kwa kutoa taarifa za uongo kwa sababu zitakwamisha juhudi za jeshi hilo.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page