BODABODA AFARIKI KWA KUCHARANGWA MAPANGA
- Fahari News
- Feb 14, 2018
- 2 min read

Dereva wa Bodaboda, Amani Mkumbo (45), mkazi wa mtaa wa Mabambasi, kata ya Ndembezi mjini Shinyanga, ameuawa na watu wasiojulikana.
Baada ya kuuawa watu hao walimnyang’anya pikipiki yake iliyokuwa na namba za usajili MC 883 BSL n akisha kuondoka nayo.
Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Shinyanga, ambaye pia ni Mkuu wa polisi wa Wilaya (OCD) Shinyanga , Claud Kanyorota, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo limetokea juzi saa 5.45 usiku katika kijiji cha Imalio, kata ya Kitangili mjini humo, ambao alikuwa amewapeleka wateja wake.
Kanyorota alisema dereva huyo alieuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani na kumcharanga kwa panga maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Alisema dereva huyo alifanyiwa unyama huo na abiria alikuwa amewapakia maarufu kama mshikaki na alifariki wakati akipelekwa kwenye matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga . “Ninachowaomba madereva wa bodaboda wachukue elimu waliyopewa na jeshi la polisi, waache kufanya kazi nyakati za usiku,” alisema Kanyorota.
Naye Ramadhani Shija, mwendesha Bodaboda alisema wimbi la mauaji na kutekwa madereva limeanza kuibuka tena kwa sababu awali lilishamiri na Jeshi la polisi lilifanikiwa kulimaliza.
Mwenyekiti wa waendesha bodaboda Mkoa wa Shinyanga, Wenceslaus Modest, alisema Mkumbo hakuwa mwanachama wao, lakini madereva wote waendesha bodaboda walikwisha pewa elimu ya kujilinda kutoendesha pikipiki nyakati za usiku.
Mke wa marehemu Josephine Kitundu, alipohojiwa alidai kuwa mume wake alikuwa na kawaida ya kurudi usiku katika kazi yake hiyo lakini juzi kabla ya tukio hilo, aliondoka kwenda kwenye kazi yake akiwa salama.
Alisema alishangaa kuona majira ya saa sita usiku baadhi ya askari wakimfuata nyumbani kwake akiwa amelala bila kumwambia chochote na kutaka aende akatoe maelezo kituo cha polisi dhidi ya mume wake.
“Nilikuwa nimelala nikasikia napigiwa hodi majira ya saa sita usiku. Nilipofungua mlango walikuwa ni askari walionifuata na kunieleza niondoke nao hadi kituoni bila kunieleza chochote.
Nilipofika waliniambia nitoe maelezo ya mume wangu ila hawakuniambia kama amefariki dunia, walichoniambia niwahi alfajili Hospitali ya Rufaa kumbe alikuwa amekwishafariki,” alisema
Comments