top of page

Askari 105 wachukuliwa hatua za kinidhamu

  • Khalidi
  • Feb 11, 2018
  • 1 min read

Bunge limeelezwa kuwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana, jumla ya askari 105 waliotenda makosa mbalimbali walichukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi. Taarifa hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum(Chadema), Sophia Mwakagenda ambaye swali lake liliulizwa kwa niaba na Mbunge wa Viti maalum(Chadema), Aida Khenani. Katika swali lake, Mbunge huyo alitaka kujua kuna sheria yeyote ya nchi inayoruhusu askari polisi kumkamata mtuhumiwa, kumpiga na kumtesa kabla hajajua kosa lake na kabla ya kufikishwa katika Kituo cha polisi. “Je, Serikali inachukua hatua zipi za kuhakikisha kuwa askari wanaofanya vitendo kama hivyo wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi?” Alihoji. Aidha alihoji kuwa mpaka sasa askari wangapi wameshachukuliwa hatua za kisheria kutokana na makosa ya kujichukulia sheria mkononi. Akijibu swali hilo, Masauni alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 Kifungu cha 11 kinaelekeza namna ya ukamataji. Alibainisha kifungu hicho mahsusi cha ukamataji hakimruhusu askari kumpiga na kumtesa raia wakati wowote anapokuwa kizuizini. Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa Kanuni za Utendaji wa Jeshi la Polisi (PGO), askari yoyote anapobainika kufanya vitendo vya kupiga au kutesa raia huchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi au kufikishwa Mahakamani. “Kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2017, jumla ya askari 105 waliotenda makosa mbalimbali walichukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi,” alisema Masauni.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page