WATEKETEZA BWENI LA WANAFUNZI 260
- Admin
- Feb 8, 2018
- 1 min read

Wanafunzi 260 wa shule ya sekondari Katunguru iliyopo Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, wamenusulika kuungua na kuteketea kwa moto baada ya bweni waliokuwa wanalitumia kuungua moto wakati wakijisomea madarasani usiku.
Tukio hilo lilitokea Feburuari 6, mwaka huu, majira ya saa 3:45 usiku.
Mwalimu Mkuu wa Shule Katunguru, Baraka Msimba jana alithibitisha kuungua hadi kuteketea kwa bweni hilo.
Alisema moto huo haukusababisha madhara kwa wanafunzi kwa sababu walikuwa darasani wakijisomea .
Msimba alieleza kuwa bweni lililoungua lilikuwa la wavulana wa kidato cha kwanza na cha pili ambalo lilikuwa na uwenzo wa kulanza wanafunzi wapatao 269 na kubainisha kuwa kati yao wanafunzi tisa walikuwa nje ya shule kwa ruhusa maalumu.
“Bweni hili lilijengwa kwa nguvu za wananchi. Tunamshukuru mungu hakuna madhara kwa wanafunzi, lakini vifaa vingine vimeteketea kw moto na hakuna kilichookolewa,” alisema.
Mkuu wa wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole jana alifika shuleni hapo kujionea tukio hilo na kueleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ya moto hakijafahamika.
Alisema jeshi la polisi litashirikiana na Zimamoto wameanza uchunguzi ili kujua chanzo chake.
Hata hivyo aliwaomba wananchi na wadau wa elimu ndani na nje ya Wilaya ya Sengerema kuwasaidia wanafunzi hao vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuendelea na masomo baada ya walivyokuwa navyo kuteketea kwa moto.
Alisema sambamba na kuanza kwa uchunguzi serikali inaendelea kufanya tathimini ya mali za wanafunzi na jingo hilo ambalo limeteketea kwa moto.
“Bado tunaendelea kufanya uchunguzi wa kubaini chanzo japo mali zote za wanafunzi zikiwemo nguo na vifaa vyao mbalimbali kama magodoro, vitanda na jingo kwa ujumla vimeteketea, hakuna kilichookolewa,” alisema.
Kommentare