top of page

HATIMA YA ZUMA KUJULIKANA KESHO.

  • Writer: Admin
    Admin
  • Feb 6, 2018
  • 2 min read

Chama tawala cha African National Congress (ANC) kitafanya mkutano wa dharura Jumatano ambao ajenda yake kubwa itakuwa kumshinikiza Rais Jacob Zuma kuachia madaraka. Hatua hiyo inakuja baada ya rais huyo ambaye heshima yake imeporomoka kukataa kujiuzulu katika vikao viwili vilivyofanyika Jumapili na Jumatatu. Shinikizo kubwa linafanyika dhidi ya Zuma ambaye utawala wake umegubikwa na kashfa za ufisadi huku akijiandaa kulihutubia taifa Alhamisi kuhusu mwelekeo wa nchi kwa mwaka 2018. Taarifa zinasema Halmashauri Kuu ya Taifa ya ANC inatarajiwa katika kikao hicho, kujadili maandalizi ya hotuba ya rais na “usimamizi wa makabidhiano ya mamlaka” kutoka kwa Zuma kwenda kwa naibu wake, Cyril Ramaphosa. Halmashauri Kuu ya Taifa ni chombo cha juu cha maamuzi ndani ya ANC na kina uwezo wa “kumwondoa” Zuma kutoka kwenye nafasi yake ya urais ingawa anaweza kukataa kutii. Mkutano maalum wa Jumatano ulitangazwa baada ya viongozi wa ngazi ya juu wa ANC kukutana kwenye makao makuu yaliyopo Jengo la Luthuli Jumatatu. Katika mkutano huo zilizuka vurugu kati ya wafuasi kindakindaki wa Zuma na wanaharakati wa mageuzi ndani ya ANC. Wanachama wengi wa ANC wanataka Ramaphosa, ambaye ni mkuu mpya wa chama, kuchukua nafasi ya Zuma, 75, kama rais mara moja. Jumatatu ya vurumai Jumatatu makundi hasimu yalivurumishana nje ya jengo hilo juu ya hatima ya Rais Zuma. Wafuasi wa kambi pinzani walikuwa wakipeperusha mabango huku wakirushiana maneno makali. Kundi mojawapo la kampeni za “Achana na Zuma” lilijikusanya nje ya jengo la Luthuli kwa lengo la kukabidhi waraka kwa viongozi wa chama wakionya dhidi ya kusudio la kumwondoa rais huyo anayepigwa vita. Kundi jingine lililokuwa na mabango yasemayo “Zuma Lazima Aondoke” lilipuuza waraka huo likisema linakwenda kutetea hadhi ya chama. Polisi walijikusanya kwa wingi nje ya makao hayo. Mfuasi mmoja wa Zuma alisema itakuwa hatari kumwondoa rais huyo kabla ya kumalizika muda wake mwaka ujao. “Tuligawanyika sana wakati ule tulipomwondoa Thabo Mbeki na sasa hatuko tayari kuona mgawanyiko mwingine, hususan kabla ya uchaguzi mkuu. Kwa hiyo tunasema ANC isithubutu kumwondoa Rais Zuma,” alisema Thabisani Mabhena. Kundi hilo linalojiita Weusi Kwanza Ardhi Kwanza ambalo linamshabikia Zuma lilisema kuwa kumwondoa rais kutasababisha mvurugano katika nchi na kunaweza kusababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe jimbo la KwaZulu-Natal (nyumbabni kwa Zuma). Muhula wa urais wa Zuma umetawaliwa na kashfa za ufisadi. Amefunguliwa kesi kadhaa ikiwemo ya kupokea malipo zaidi ya 783 katika kesi anayohusishwa kuingia mkataba mbovu wa ununuzi wa silaha kabla ya kuwa rais mwaka 2009. Madai mengi ya udanganyifu yamemshona akihusishwa na familia tajiri ya Gupta ambayo inatuhumiwa kutumia hila kujipatia miradi minono ya serikali na kupewa fursa ya kuchagua nafasi za kuteuliwa kwenye uwaziri. Profesa wa siasa wa Chuo Kikuu cha Johannesburg Mcebisi Ndletyana ameelezea uwepo wa Zuma kuwa ni "hasara kubwa" kwa ANC

Commentaires


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page