KAMA SI DOCTOR… OKWI ANGEPOTEZA MAISHA
- Fahari News
- Feb 5, 2018
- 2 min read

Hofu kubwa ilitanda kwa muda Simba baada ya Straika Emmanuel Okwi kupigwa ngumi uwanjani jana na kuzimia kwa muda.
Okwi alipigwa ngumi ambayo haikujulikana mara moja kama bahati mbaya katika mchezo wa ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Okwi ambaye ni mchezaji tegemeo Simba akiwa kileleni mwa chati ya wafungaji na mabao yake 12, alipigwa ngumi ya nguvu na beki wa kushoto wa Ruvu Shooting, Mau Bofu dakika ya 45 na kuanguka chini.
Beki huyo ni mwajiliwa wa jeshi la kujenga Taifa akiwa na hadhi ya Private, na baada ya rafu hiyo alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Akiwa chini, Okwi alionekana kupoteza fahamu kwa zaidi ya dakika moja, kisha baadaye dakitari wa Simba, Yassin Gembe akakimbia uwanjani na kumsukumiza maeneo ya kifua ili kurudisha pumzi yake, hatua ambayo ilifanikiwa.
Hata hivyo hali haikuwa nzuri kwa Okwi ambaye hakuweza kuendelea na mchezo huo na alipotoka alielekea moja kwa moja kwenye benchi, lakini baada ya mechi alifuata ili kuzungumza naye akidai kwa ishara kuwa hawezi kuzungumza chochote kwa kile kilichoonekana ni maumivu.
Daktari alifanya kazi ya ziada kuokoa maisha yake kwa kumtikisa na kurudisha hali yake.
Hata hivyo baada ya mechi, daktari huyo alisema kuwa Okwi atakuwa fiti kuivaa Azam FC keshokutwa Jumatano katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
“Hakuna shida ya Okwi kucheza mechi ya Azam Jumatano. Hana tatizo lolote,” alisema Gembe.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, alisema kuwa anaamini Ruvu Shooting walipania kuwaumiza wachenzaji wao mahiri wakiwemo John Bocco na Okwi kwa kuwa walicheza rafu za mara kwa mara.

“Walikuwa wakicheza rafu nyingi za mara kwa mara, unaweza ukasema kwamba walipania kuwaumiza wachezaji wetu,” alisema Hans Poppe.
Katika mchenzo huo wa jana, Simba ilishinda mabao 3-0 na kuendeleza umwamba wao wa ligi Kuu Bara msimu huu wakiwa wamefunga mabao 15 katika mechi tano zilizopita.
Comments