top of page

WANAWAKE WAWILI WAUAWA KWA IMANI ZA KISHIRIKINA

  • Fahari News
  • Jan 31, 2018
  • 2 min read

Watu watatu wameuawa katika matukio tofauti, likiwamo la wanawake wawili ambao walikatwa mapanga kutokana na imani za kishirikina.

Tukio la kuuawa wanawake hao lilitokea usiku wa kuamkia jana saa 8:00 usiku, katika Kitongoji cha Kilombero Katuntu, Kijiji cha Chalachima, Kata na Tarafa ya Chala wilayani Nkasi, Mkoa wa Rukwa. Kamanda wa polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, aliwataja marehemu hao kuwa ni Salome Kisinza (50) na Rahel pawa (22), ambao walikatwakatwa na mapanga katika sehemu mbalimbali za miili yao na watu wasiojulikana.

Alisema kuwa, waliofanya mauaji hayo waliwavizia wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao, ndipo walipovunja mlango na kuingia ndani na kuanza kuwakata mapanga.

Baada ya tukio hilo watuhumiwa walitoweka wakiwa wamemuua Salome na kumjeruhi Rachel na kumuacha mahututi, lakini alifariki baadaye akiwa njiani kupelekwa hospitali kwa matibabu.

Kamanda Kyando alisema chanzo cha mauaji hayo inasemekana ni imani za ushirikina, kwakuwa mmarehemu Salome allikuwa anatuhumiwa kumroga mume wake aitwaye Jilala Mponeja, ambaye, ambaye anaumwa kwa muda mrefu na anaendelea na matibabu kwa mganga wa jadi wilayani Kalambo mkoani humo.

Inadaiwa kuwa marehemu Salome aliolewa na Mponeja baada ya kufiwa na mkewe na inasemekana kuwa watoto wake ndio waliopanga njama za mauaji hayo. Kwani walikuwa wanamtuhumu kuwa ndiye aliyemloga mama yao ili yeye aolewe na baba yao.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la polisi linaendelea na msako ili kuwakamata watuhumiwa hao. Kamanda Kyando alisema katika tukio jingine lililotokea siku hiyo saa 3:00 usiku katka shule ya sekondari Tawheed, Kata ya Izia, Tarafa ya Lwiche, Manispaa ya Sumbawanga, mtu aliyefahamika kwa jina moja la Hassani (27), mkazi wa Kizwite, aliuawa kwa kipigo akituhumiwa kuiba bomba moja la chuma lenye urefu wa futi 10 na misumari kilo moja na nusu pamoja na kipande cha bati ambavyo thamani yake bado haijajulikana.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page