WALIOVUA NGUO KORTINI WAFUNGWA MIEZI 6 JELA
- Fahari News
- Jan 31, 2018
- 2 min read

Watuhumiwa 24 kati ya 61 wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi na ulipuaji mabomu jijini Arusha, wamehukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kuvua nguo na kisha kugoma kuingia ndani ya chumba cha mahakama kusikiliza kesi zinazowakabili.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Nestori Baro wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha na kusema kuwa, watuhumiwa hao wa ugaidi wamehukumiwa kwa mujibu wa kifungu Nambari 114 (a) cha Mwongozo wa Mashtaka ya jinai.
Hata hivyo, baada ya hukumu hiyo baadhi ya watuhumiwa walitenda tena utovu wa nidhamu kwa kuamua tena kuvua nguo zao za ndani wakati wakipandishwa kwenye karandinga wakirejeshwa katika gereza Kuu la Mkoa wa Arusha lililopo Kisongo nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Awali kabla ya kusoma hukumu hiyo Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Augustino Kombe, aliiomba mahakama hiyo iwachukulie hatua kali na kutoa adhabu kwa watuhumiwa wa kesi hizo wanaogoma kuingia mahakamani kutajwa kesi yao. Hakimu Baro alisema kwamba anaotoa kifungo cha miezi sita kwa watuhumiwa hao ili iwe fundisho kwa wengine watakaonesha vitendo hivyo alivyosema siyo vya kistaarabu.
Waliohukumiwa ni Rajabu Yakubu, Swalehe Hassan , Anwar Mashali, Jafari Lema, Abdul Hamid, Mgaya Mgayaa, Abdallah Rabia, Hassan Said, Abdalah Juma, Maka Gewa, Sudi Nassib na Swalehe Hamis. Wengine ni Hamad Issa, Yassin Mohammed, Hamad Yahya, Juma Nguli, Khalid Makame, Shaban Wawa, Yassin Sanga, Ally Hamis, Ibrahim Lend, Rajab Hemed, Shaban Masu sanjari na Mahammed Nuru.
Mara baada ya kutoa hukumu hiyo Hakimu Baro aliahirisha kesi inayowakabili watuhumiwa hao hadi Februari 13, mwaka huu kwa maelezo kwamba upelelezi juu ya shauri lao bado haujakamilika.
Watuhumiwa hao 61 wanakabiliwa na kesi ya kujihusisha na vitendo mbalimbali vya kigaidi ambapo kati yao hao watuhumiwa 23 wanatuhumiwa kwa kesi ya ugaidi nyumbani kwa Sheikh Sudy Ally Sudi Januari 13, mwaka 2014.
Comments