WAWEKEZAJI VODACOM WAPOTEZA SH 350 BILION
- Fahari News
- Jan 29, 2018
- 2 min read

Wawekezaji wa kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom Tanzania wamepoteza mtaji wa sh 350 bilioni katika kipindi cha miezi mitano, tangu kuorodheshwa kwenye soko la Hisa Dar es salaam (DSE). Ripoti za soko hilo zinaonyesha kwamba, mtaji wa soko wa kampuni hiyo umepungua na kufikia sh 1.6 trioni mwishoni mwa wiki iliyopita, kutoka sh 2 trioni agosti mwaka jana
Kushuka kwa mtaji wa soko ni matokeo ya kupungua kwa bei ya hisa za kampuni hiyo hadi kufikia sh 740 baada ya soko la Alhamisi wiki iliyopita, kutoka sh 850 za Jumatano.
Kushuka kwa bei ya hisa za Vodacom Tanzania kwa kiwango hicho ni matokeo ya uuzaji wa asilimia 0.1 ya hisa zote zilizoorodheshwa kwenye soko.
Bei ya hisaa za Vodacom Tanzania ambayo iliorodhesha hisa zake kwenye soko hilo miezi mitano iliyopita, ilifikia kiwango cha juu cha sh 900 siku ya kuorodhesha Agosti 15 mwaka jana.
Hii inamaana kwamba mwana hisa aliyenunua hisa 1000 kwenye kipindi cha toleo la awali (IPO) KWA SH 850,000, uwekezaji huo ulipungua hadi kufikia sh 740,000 wiki jana.
Ripoti za DSE zinaonyesha kwamba wawekezaji wa kampuni hiyo waliuza na kununua hisa kwa sh 730 Alhamisi iliyopita, japo bei ya kufungua na kufunga mnada ikiwa n ash 740.
Wachambuzi wanasema kushuka kwa bei ya hisa za kampuni hiyo huenda ikawa kawaida, kwani inasababishwa na wingi wa hisa za kuuza na uchache wa wanunuzi.
Ripoti za DSE zinaonyesha kwamba idadi ya hisa zinazowekwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa katika kipindi chiki ni nyingi zaidi ya mahitaji kuuza kwa bei ndogo.
“Kushuka na kupanda kwa bei ya hisa ni jambo la kawaida, lakini sababu kubwa huwa ni kuwapo kwa idadi ya hisa zinazohitajika kuuzwa,” alisema Juvenary Simon, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Orbit Securities Limited kampuni ambayo ni washauri wa uwekezaji DSE.
Vodacom Tanzania ambayo inaongoza kwa idadi kubwa ya wateja kwa kampuni za simu za mkononi kwa upande wa mawasiliano na huduma za kifedha, inatarajia kufunga mwaka wake wa fedha Machi.
Commentaires