BODI ZA SHULE WASUSA VIKAO, KISA POSHO
- Fahari News
- Jan 29, 2018
- 2 min read

Baada ya serikali kupinga vikali michango shuleni, kumeleta sura mpya baada ya wajumbe wa bodi za shule kususia na kushindwa kuhudhuria vikao mbalimbali bila kulipwa posho, hivyo kukwamisha maendeleo mkoani Mtwara.
Hali hiyo imebainika baada ya wajumbe wa mradi wa ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma katika sekta ya elimu Manispaa ya Mtwara Mikindani kutoka Shirika la Faidika wote kwa pamoja (Fawopa) kutembelea shule mbalimbali na kubaini kusimama kwa maamuzi mengine katika shule hizo.
Akizungumza katika kikao cha wadau wa elimu kilichoandaliwa na Fawopa kwa kuwakutanisha maofisa watendaji kata, walimu wakuu, wachumi, wazazi na maofisa elimu, Mratibu wa shirika hilo, Baltazar Komba, alisema vikao vingi vilisimama baada ya Serikali kutoa agizo la elimu bure.
Alisema hali hiyo imetokana na kutokuwepo kwa michango shuleni na wajumbe hao kukosa posho ya kujikimu, hali ambayo inawafanya walimu wachukue uamuzi wenyewe.
“Unajua serikali imefanya mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu, lazima tulitambue hilo na tujue nini kifanyike kwa ajili ya maendeleo ya shule zetu, tunaamini kuwa wenye mamlaka wapo wakemee hii hali inayoendelea ya kusimama kwa vikao vya bodi za shule kutokana na kukosa posho, huku ni kujirudisha nyuma katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
“Hivi vikao vya bodi za shule visipoendelea, maamuzi yatakuwa yanatolewa upande wa walimu tu, hali ambayo inaweza kuchangia kudorora kwa elimu nchini na kusimama kwa maendeleo ya shule zetu, tushirikiane kuzikumbusha mamlaka kuchukua hatua ili vikao hivi virudi na maamuzi yachukuliwe.”
“Mimi nipo kwenye bodi mojawapo ya shule ya msingi, naona mahudhurio ya wajumbe yanavyoshuka kila siku, wapo wajumbe ambao wanahudhuria vikao vya maamuzi kwa ajili ya maendeleo ya shule vimesimama, hii ni hatari zaidi kwa mustakabali wa elimu nchini,” alisema Komba.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari Sabasaba, Musa Muponda, alisema hivi sasa hali si nzuri kwani vikao bodi za shule havifanyiki.
“Kikifanyika kikao kimoja wajumbe 15 wanapaswa wahudhurie ambapo wanalipwa Shilingi 70,000 kwa kila mmoja, changamoto inakuja shule hazina miradi na miradi iliyopo haiwezi kusaidia kutatua hilo, hali inayopelekea vikao kusimama na pale maamuzi yanapohitajika kufanywa na walimu,” alisema Mponda.
Comments