MAISHA YA 'NABII TITO NA FAMILIA YAKE' NDANI YA CHUMBA KIMOJA
- Fahari News
- Jan 25, 2018
- 2 min read

Wakati polisi mkoani Dodoma ikiendelea kumshikilia Tito Machibya, maarufu Nabii Tito, kwa madai ya kudhihaki dini ya Kikiristo, waandishi wa habari wamefika nyumbani kwake na kuelezwa kuwa mtu huyo anaishi kwenye chumba kimoja na mkewe, watoto wake watatu na binti wa kazi ambaye amekuwa akitangaza kwamba amezaa naye pia.
Tito amekuwa akizunguka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam na Dodoma, ikiwamo kwenye vilabu vya pombe, akiwa na biblia huku akihubiri kwamba kunywa pombe na kuzaa na mfanyakazi wa ndani si dhambi.
Hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii, ilisambaa video iliyomuonyesha Tito akiwa jukwaani na mkewe, mfanyakazi wake wa ndani huku wakinywa pombe, kucheza mziki wakati mwingine akinyonyana ndimi na mfanyakazi huyo na mkewe.
Baada ya Tito kukamatwa juzi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, kupitia ukurasa wake wa Twitter, aliandika: “Udhalilishaji wa aina yoyote ile haukubaliki (Kijinsia, Dini n.k).”
Baada ya juzi kusema polisi wamempeleka Tito Hospitali ya Mirembe na amegundulika kuwa na matatizo ya akili
Kwa mujibu wa Erika Mapuluti ambaye ni mpangaji mwenzake, Tito, amekuwa akiishi chumba kimoja na mke wake ambaye ambaye anamtaja kwa jina moja la Agnes pamoja na watoto wake watatu na mfanyakazi wake wa ndani.
“Hiki chumba unachokiona anaishi yeye, mke wake, watoto wake watatu na mfanyakazi wake wa ndani, huwa hatumwelewi, lakini ndiyo maisha aliyoyachagua yeye na sisi huwa hatufuatiliani, kila mtu na maisha yake.
“Mlango kama unavyouona ni mbovu, hivyo hapa kaweka pazia tu na ukiingia ndani unaona kila kitu jinsi alivyokuwa akiishi chumba kimoja na mke wake na watoto wake,” alisema Erika.
Alisema kwamba wameishi nae kwa zaidi ya mwaka mmoja, lakini kwa sasa kutokana na sekeseke hilo, wameamua kuhama kwani wanaona wanaishi na mtu ambaye si mstaarabu.
“Tunahama sasa hivi na mume wangu, kapata chumba, tunahamia ule mtaa wa kule juu, hatutaki na sisi kushiriki hii dhambi, tulikuwa hatuelewi kitu, lakini sasa hivi tumeelewa kutokana na kuona amekamatwa.”
Comments