SIRI YA KUGONGWA NA NDEGE NA KUFARIKI
- Fahari News
- Jan 23, 2018
- 1 min read

Kamanda wa polisi wa Viwanja vya ndege nchini, Matanga Mbushi, ameweka bayana chanzo cha mwanamke aliyegongwa na ndege ya Fastjet Jijini Mwanza na kufariki dunia kuwa alikuwa na matatizo ya akili.
Akizungumza jana kamanda Mbushi alisema hadi sasa wameshindwa kubaini jina la mwanamke huyo ambaye alifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na ndege.
Ajali hiyo ilitokea katikati ya wiki iliyopita usiku kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, uliopo wilayani Ilemela.
Ndege hiyo ilimgonga mwanamke huyo akiwa anavuka kwenye njia ya kurukia ndege wakati ndege hiyo yenye namba za usajili 58S-EJE190 ikiwa kwenye mwelekeo wa kuruka.
Alipoulizwa kama mwanamke huyo amefahamika na hatua gani zinachukuliwa ili tukio hilo lisitokee tena, Kamanda Mbushi alisema wanaopaswa kuzungumzia hilo ni mamlaka ya usalama wa Anga (TCAA).
“Yule mwanamke bado hatujapata jina lake, lakini anavyoonekana kuwa alikuwa na matatizo ya akili,” alisema.
Akizungumza kamanda huyo alisema wakati ndege hiyo ikiwa kwenye mwerekeo wa kuruka mwanamke huyo alikuwa anakatiza kwenye njia ya ndege ndipo alipogongwa na kufa papo hapo.
“Ndege hii ilikuwa kwenye mruko wa futi 148 tokea pointi 12 kuelekea pointi 30 ikiwa na abiria 89 waliokuwa wakitokea Mwanza kwenda Dar es salaam.
Alisema pamoja na ajali hiyo, ndege hiyo iliruka na kusafiri salama hadi Dar es salaam.
Comentários