WATUHUMIWA WA KESI ZA UGAIDI WAVUA NGUO MAHAKAMANI
- Fahari News
- Jan 17, 2018
- 1 min read

Baada ya mahabusu wanaokabiriwa na tuhuma za ugaidi, walizua tafrani katika viwanja vya mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Arusha baada ya kuvua nguo wakipinga kuchelewa kukamilika kwa upelelezi wa kesi zao.
Waliovua nguo ni kati ya watuhumiwa 61 wanaokabiliwa na tuhuma hizo za ugaidi na ambao wako katika gereza la Kisongo.
Kabla ya kushuka kutoka kwenye karandinga baada ya kufika Mahakamani hapo saa 3:30 asubuhi, baadhi yao walivua nguo na kusababisha utaratibu wa kuwapeleka chumba cha mahabusu kabla ya mahakamani kuingia dosari.
Askari magereza walilazimika kuimarisha ulinzi mahakamani hapo huku wakiendelea na jitihada za kuwataka wavae nguo zao lakini waligoma na hivyo kulazimika kuwapeleka chumba hicho wakiwa hawajavaa chochote.
Baada ya kuwafikisha mahabusu na kuwaacha huko, askari hao waliwachukua watuhumiwa ambao hawakuwa wamevua nguo na kuwapeleka mahakamani kusikiliza shauri lao.
Pamoja na kufanya kituko hicho kupinga kucheleweshwa kwa upelelezi, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinda aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 30 kutokana na upelelezi kutokamilika.
Mara baada ya kuahirisha shauri hilo watuhumiwa hao walirudishwa ndani ya chumba cha mahabusu ambako walikaa humo kwa muda na wenzao waliokuwa wamevua nguo kabla ya kupandishwa kwenye karandinga kurejea Kisongo.
Comments