ANAYEDAIWA KUUA MKE, MTOTO, SHEMEJI AKAMATWA IRINGA
- Fahari News
- Jan 17, 2018
- 2 min read

Jeshi la polisi linamshikilia mhasibu wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Lucas Lukule anayetuhumiwa kuua mke, mtoto na shemeji yake kwa kile kilichodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 14 akiwa mkoani Iringa na Jeshi la polisi linafanya utaratibu wa kumrejesha Dar es salaam ili kufunguliwa mashtaka.
Tukio hilo lilitokea Januari 4 nyumbani kwake eneo la Goba Matosa , Lukule anatuhumiwa kuchukua uamuzi huo baada ya kumtuhumu mkewe kwa muda mrefu kuwa mtoto wa miezi minne si wa kwake na kwamba anajihusisha na mapenzi na wanaume wengine.
Polisi alidai kuwa alikuta ujumbe wa Kukule eneo la tukio, akishauri mtu yeyote asihusishwe mauaji hayo kwa kuwa yeye ndiye aliyefanya.
Kamanda wa polisi kanda Maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa alisema kuwa baada ya kuhojiwa, mtuhumiwa huyo alikiri kufanya mauaji hayo kutokana na kumtuhumu mkewe anayeitwa Upendo kuzaa mtoto na mwanaume mwingine.
“Leo ni siku ya tatu tangu tumkamate Lukule na tunafanya utaratibu wa kumleta hapa jijini Dar es salaam,” alisema.
“Tulipomuhoji alitueleza vizuri jinsi alivyotumia jembe kumuua mke wake Upendo, Mtoto wa miezi minne pamoja na shemeji yake anayeitwa Magreth.”
Awali, mjumbe wa serikali ya Mtaa wa Goba Matosa, Hamidu Pondomo alisema siku ya tukio, kaka wa marehemu alienda nyumbani kwa dada yake ambako alitumwa na mama yake baada ya kushindwa kumpata kwa simu.
Alisema ndugu huyo aliwaeleza kuwa Lukule alimpigia simu mama huyo siku ya tukio, lakini hakuzungumza chochote.
“Mama wa marehemu alipoona Lukule amepiga simu bila kuzungumza chochote, alipiga simu ya Upendo ikawa inaita bila majibu, ndipo alipoamua kumtuma mtoto wake wa kiume kwenda kumtazama,” alisema Pondomo.
Alisema alipofika alikuta mlango umefungwa na alipochungulia dirishani aliona miili mitatu sakafuni ikiwa imetapakaa damu.
“Baada ya hapo ndipo taarifa zikatolewa polisi ambao walifika na kuvunja mlango. Walikuta mwili wa Magreth sebuleni ukiwa na jeraha kubwa kichwani, mwili wa Upendo na mtoto ukiwa chumbani. Wao pia walikuwa na majeraha kichwani,” alisema.
Comments