MTOTO ALIYETEKWA NA ‘WAUAJI’ ATOROKA
- Fahari News
- Jan 16, 2018
- 1 min read

Mtoto aliyetekwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wauaji katika Kijiji cha Remng’orori, Waibe Wigesa (12), amepatikana huku hali ya hatari ikijirudia baada ya kundi hilo la watu zaidi ya 15 kuwakimbiza tena wananchi wa kijiji hicho.
Wigesa alitekwa na kundi la watu zaidi ya 40 kutoka Mikomarilo (Wakurya) siku ya Januari 12, mwaka huu wakati baba yake, Wigesa Kigene na Mwikwabe Nghebo waliuawa kwa kukatwa katwa na mapanga, shoka na kuchomwa mishale
Akizungumza akiwa eneo la tukio, mkazi wa Mentoha, Kijiji cha Remng’orori, Juma Kitang’ita, alisema akiwa na wananchi wengine katika mashamba yao, ghafla yowe lilisikika karibu nao na walipotahamaki waliona kundi la watu zaidi ya 15, lakini aliweza kuwatambua wawili kwa majina yao, Isaka Rioba na Machandi Matiko.
“Mkuu wa Mkoa na polisi walikuja hapa tangu tukio lilipotokea, walilinda kwa siku mbili na jana waliondoka na kutuhakikishia hali ni shwari, hivyo sisi tuliendelea kufanya shughuli zetu tukijua usalama upo, lakini hali imejirudia.
“Kundi hilo wengi ni vijana ambao walikuwa wamevaa mashati yaani wapo kifua wazi, sasa hapa tulipo tumejikusanya tunasubiri polisi maana Mwnyekiti wa Kijiji, Herzon Nganyi ametoa taarifa polisi polisi,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu, alikiri tukio la kukimbizwa wananchi wa Remng’orori na alituma askari polisi wakiongozwa na Mkuu wa polisi wa Wilaya (OCD).
“Ni kweli nimepigiwa simu na Mwenyekiti wa Kijiji cha Remng’orori kuwa hali ya usalama si nzuri baada ya kundi la vijana kuibuka, nimemwambia atangulie eneo la tukio, nimewasiliana na mkuu wa wilaya ya Bunda na OCD wake, tumekubaliana kupeleka askari pale, bila shaka wapo njiani kwa sasa,” alisema Babu.
Comments