JPM apokea taarifa ya Airtel,
- Khalidi
- Jan 12, 2018
- 1 min read

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amewasilisha taarifa ya kamati aliyoiunda kuchunguza umiliki wa Kampuni ya Simu ya Airtel kwa Rais John Magufuli, aliyeagiza kufanyika kwa uchunguzi huo Desemba 20, mwaka jana.
Akiwasilisha taarifa yake, Dk Mpango alisema Serikali imejiridhisha kuwa ubinafsishaji wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kwenda Celtel, baadaye kuhamishiwa Zain na sasa Airtel, ulifanyika kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu. Kufuatia ukiukwaji huo, Dk Mpango alisema Serikali inayomiliki asilimia 40 ya hisa za kampuni ya Airtel, imeamua kufanya mazungumzo na kampuni ya Airtel inayomiliki asilimia 60 ya hisa ili nchi iweze kupata haki yake.
“Lakini niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya hovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi zimepotea kwa hiyo sisi katika majadiliano haya, lengo letu litakuwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao,” alisema Dk Mpango.
Taarifa nyingine iliyowasilishwa kwa Rais ni ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Novemba 25, mwaka jana wakati wa ufunguzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (Mloganzila) kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Baadhi ya maagizo hayo ni kupunguza baadhi ya idara na madaktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuhamishia Mloganzila na hospitali za mikoa kuhamishwa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Waziri Ummy aliwasilisha taarifa hiyo, akiwa ameongozana na viongozi wakuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (MUHAS).
Comments