POLISI YAONGOZA KUDAIWA MAJI DODOMA
- Fahari News
- Jan 9, 2018
- 1 min read

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa), David Pallagyo, amesema malimbikizo ya madeni ya Ankara za maji ni zaidi ya Tsh Bilioni 1.8, huku jeshi la polisi likiongoza kwa deni la Tsh. Milioni 600.
Pallagyo alisema hayo wakati akitoa taarifa fupi ya utendaji kazi wa Mamlaka hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, DK, Binilith Mahenge, pamoja na mikakati ya kuongeza uzalishaji maji ili kukidhi ongezeko la watu kutokana na ujio wa makao makuu.
Alisema madeni makubwa katika taasisi za serikali yanayolimbikizwa ni kikwazo kikubwa katika kuongeza ufanisi wa uzalishaji wa huduma ya maji.
Alisema katika deni la Sh. Bilioni 1.8 linatokana na taasisi mbalimbali za serikali mkoani hapo, Jeshi la polisi linaongoza kwa kuwa na deni la Sh. Milioni 600 hadi hivi sasa.
“Mkurugenzi kama kuna watu wanaodaiwa naomba niletee majina yao ofisini kwangu, mimi nitawaita waje waseme wanalipa lini zoezi kama hili nilishalifanya hata wakati nikiwa Ruvuma,” alisema DK. Mahenge.
Hata hivyo, aliitaka mamlaka hiyo kujikita zaidi katika kutekeleza mikakati yake ya muda mfupi ili kuongeza vyanzo vya maji ambavyo vitasaidia kukidhi mahitaji ya watu ambao wanahamia Dodoma kwa kasi kkubwa kutokana na ujio wa makao makuu.
Comments