TANZANIA YAKUMBWA NA UHABA WA SAMAKI
- David
- Dec 26, 2017
- 2 min read

Idadi ya samaki katika Bahari ya Hindi nchini Tanzania imepungua kwa kasi, huku lawama zikitolewa kwa wale wanaoendesha shughuli za uvuvi kwa njia ambazo si halali.
Ripoti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyotolewa hivi karibuni imeonyesha kuwa wavuvi haramu hutumia njia zisizo halali kuvua katika maeneo yenye kina kirefu. Miongoni mwa njia wanazotumia ni pamoja na kutumia baruti, mafuta, na nyavu zenye matundu madogo, lakini pia kuvua kupita kiasi.
Inakadiriwa kuwa, idadi ya samaki waliovuliwa kwa mwaka 2016 imeporomoka hadi tani 360,000 kutoka wastani wa tani 390,000 katika miaka minne iliyopita. Tanzania inauhitaji wa jumla ya samaki tani 730,000 kwa mwaka.
Kampuni za ndani sasa imeamua kuagiza samaki kutoka nchini China, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa tani 2,000 za samaki aina ya Mackerel huingia nchini Tanzania kila mwezi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalla Ulenga amesema kuwa serikali ipo katika mkakati wa kuzuia matumizi ya baruti katika uvuvi kutokana na kuwa huharibu hadi mazalia ya samaki. Aidha, amesema pia wizara itajikita katika kutoa elimu kwa wavuvi kuhusu njia bora ya kuvua samaki.
Serikali ya Tanzania inawahimiza wavuvi kuunda vikundi ambapo kupitia vikundi hivyo itaweza kutoa ruzuku ya asilimia 40 ya gharama zinazohitajika kwa ajili ya kununu vifaa vya kisasa kwa ajili ya uvuvi.
Ripoti ya mwaka 2017 iliyotolewa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) imesema kuwa uvuvi haramu bado ni changamoto kubwa Magharibi mwa Bahari ya Hindi, hali inayosababisha Tanzania kupata hasara ya Tsh 898 bilioni kwa mwaka.
Spika wa Bunge, Job Ndugai ameunda kamati ya watu 8 kuchunguza kuhusu vifaa vya uvuvi ambapo itaishauri serikali kuhusu hatua bora za kuchukua kuweza kunufaika na bishara ya uvuvi.
Kamati hiyo ambayo iliundwa mwezi Novemba, pia itafanya uchunguzi wa hasara ambayo taifa linapata kutokana na uvuvi usiozingatia sheria.
Ndugai wakati akiunda kamati hizo alisema kuwa, taifa linanufaika kwa asilimia ndogo sana kutokana na biashara ya uvuvi tofauti na mataifa mengine ambayo yanapakana na bahari ya hindi au Atlantic.
Spika alitolea mfano wa Namibia ambapo sekta ya uvuvi inachangia asilimia 10 ya Pato la Taifa wakati nchini Tanzania sekta hiyo inachangia asilimia 1.4 tu.
Ndugai alisema kuwa Tanzania hupoteza shilingi bilioni 400 kila mwaka kutoka katika bidhaa za samaki.
Comentarios