Wafanyabiashara Jijini Walalama Kukosa Wateja
- Khalidi
- Dec 24, 2017
- 1 min read

Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo jijini hapa, wamelalamikia ugumu wa biashara katika kuelekea sikukuu ya Krismasi wakidai kukosa wateja. Mmoja wa wafanyabiashara hao anayeuza nguo, Athumani Mhina alisema sikukuu ya mwaka huu iko tofauti na ile ya mwaka jana ambayo biashara ilikuwa inatoka. “Mwaka jana biashara ilikuwa afadhali japokuwa tangu awamu hii ya tano imeanza wateja wamepotea hali inayosababisha kukaa na nguo muda mrefu na wakati mwingine tunauza kwa bei ya hasara,” alisema. Akizungumzia maandalizi ya sikukuu, Mwajuma Shabani alisema sikukuu ya mwaka huu itakuwa ngumu kwa kuwa hata fedha kwa ajili ya kununulia familia yake nguo zimekuwa ni ngumu kuzipata. “Nimekuwa nakuja hapa tangu wiki iliyopita kuangalia nguo za watoto, lakini kila nikija bei zipo juu, sielewi watoto watasherehekeaje sikukuu mwaka huu,” alisema. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Philimini Chonde alisema biashara imekuwa ngumu kutokana na wateja kupungua.
Comments