POLISI WAMUOKOA KIKONGWE
- Fahari News
- Dec 22, 2017
- 2 min read

Jeshi la polisi mkoa wa Mbeya, limefanikiwa kuzima jaribio na vurugu alizofanyiwa kikongwe Ngavagila Ngogo (93) na wajukuu wake wanane waliomvamia nyumbani kwake, kumtoa ndani kibabe na vitu vyake kutupwa nje bila kufuata sheria.
Kamanda wa polisi mkoa Mbeya alisema kuwa jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa raia wema, kwamba dalari mmoja akiwa ameongozana na kundi la vijana, wakiwamo wajukuu wanane wamemvamia bibi yao kwa nia ya kumtoa ndani ya nyumba yake.
Alisema baada tya kufika eneo la tukio waliweza kuzuia kitendo cha bibi huyo kutolewa ndani katika nyumba iliyouzwa na wajukuu hao wakiongozwa na mtu aliyetajwa kuwa ni msimamizi wa mirathi Apolo Ngajilo.
Kamanda mpinga alisema kuwa baada ya uchunguzi wa mahojiano waliyoyafanya waligundua kuwa dalali aliyepewa kazi hiyo hana kibali chochote cha kisheria na hajapewa agizo hilo na mahakama.
“Nilichokifanya haraka ni kuhakikisha jeshi la polisi limekwenda kuweka usalama katika nyumba hiyo na kuzuia bibi huyo na vitu vyake vibari ndani hadi hapo amri ya mahakama itakapotolewa kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema kamanda Mpinga.
Alisema kwa dalali aliyekodiwa kufanya kazi hiyo, amekamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi kituo kikuu cha polisi kwa mahojiano zaidi, licha ya kukiri awali kuwa hana kibari wala amri yoyote ya mahakama iliyompa kazi hiyo.
Kamanda Mpinga alisema kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi mwingine ili kuweza kubaini uhalali wa dalali huyo na kampuni inayomtuma kuendesha kazi ya kutoa vitu vya bibi huyo na kumtoa nje kinguvu.
Sakata la bibi huyo, limetokea kwenye nyumba yake aliyoanza kuishi tangu mwaka 1973 baada ya kununua eneo hilo kama shamba mwaka 1968 maeneo ya mwanjelwa, ambako sasa wajukuu zake wanamtaka atoke ndani wakidai kuwa mali hiyo ni ya baba yao, marehemu Peter Ngajilo, mtoto wa pili wa kikongwe Ngavagila.
Comments