top of page

MWEKEZAJI VINGUNGUTI APEWA SAA 12 KURUDISHA NYARAA ZA WANANCHI

  • Khalidi
  • Dec 22, 2017
  • 2 min read

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametoa saa 12 kwa Meneja wa Kampuni ya PMM ya Dar es Salaam, Deogratius Chacha kurejesha nyaraka za umiliki wa ardhi, zilizochukuliwa na kampuni hiyo kwa wakazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam ili kuchukua maeneo yao, vinginevyo akamatwe na Jeshi la Polisi.

Lukuvi amemwagiza meneja huyo kuwarudishia nyaraka hizo hadi ifikapo kesho saa tano asubuhi. “OCD chukua vielelezo vya Meneja, hakikisha hadi kufikia kesho saa tano awe amewarudishia wananchi nyaraka zao, kinyume cha hapo mkamateni mmuweke ndani,” amesema Waziri Lukuvi.

Katika hatua nyingine, Lukuvi amefanikiwa kuumaliza mgogoro huo wa ardhi wa muda mrefu kati ya wakazi wa Mtaa wa Mtambani Vingunguti na mwekezaji huyo wa Kampuni ya PMM ya Dar es Salaam.

Mwekezaji huyo wa Kampuni ya PMM inayojihusisha na uhifadhi wa mizigo, alitaka kuchukua eneo la ekari 228 lenye nyumba 4,000 na wakazi 70,000 wa Mtaa wa Mtambani Vingunguti. Waziri Lukuvi alisema serikali

haitambui uwekezaji uliokuwa ufanyike na kwamba, mwekezaji hakufuata utaratibu uliowekwa na serikali, hivyo kusababisha mgogoro huo kuwa mkubwa.

Kwa mujibu wa wananchi wa eneo hilo, tangu mwaka 2012 mwekezaji huyo aliwazuia kufanya shughuli zozote za uendelezaji, kwa kile alichodai ameshafanya tathmini na anaisubiri Wizara ya Ardhi ambayo inamchelewesha, jambo ambalo Lukuvi alikanusha.

Mwekezaji huyo ametakiwa kurejesha nyaraka alizozichukua kwa wananchi hao kinyume na utaratibu na ametakiwa kuwalipa fidia wananchi, kwa kuwa aliwazuia kufanya shughuli zozote za uendelezaji, kwa kile alichodai ameshafanya tathmini. Hata hivyo, hadi sasa hakuna kinachoendelea na malipo hayajafanyika.

Lukuvi aliwaambia wananchi hao kuwa kuanzia leo, haya maeneo ni mali ya wananchi kama anataka kununua aanze upya kufuata utaratibu uliowekwa, na haiwezekani mtu anakuja kuwanunua watu 70,000 kienyeji.

“Hatuzuii mtu kuuza mali yake, tunachosimamia sisi ni haki itendeke na utaratibu ufuatwe, lakini katika mchakato huu mambo yamekwenda ndivyo sivyo,” alisema Waziri Lukuvi. Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa PPM, Chacha alisema wapo katika hatua za mwisho na malipo yangefanyika ndani ya siku 90 zijazo, lakini kwamba wananchi hao hawakukubaliana na hilo.

Wakazi wa eneo hilo walimwambia Lukuvi kuwa mwekezaji huyo alichukua pia leseni zao za makazi kwa muda mrefu, hivyo kushindwa kuendeleza makazi yao. Hata hivyo, hadi sasa hakuna kinachoendelea na malipo hayajafanyika zaidi ya ahadi za mwekezaji huyo kwamba anasema Wizara ya Ardhi ndiyo inayomchelewesha

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page