JAMES MBATIA APATA AJALI, AVUNJIKA MKONO
- Fahari Neews
- Dec 21, 2017
- 1 min read

Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR- Mageuzi), amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi mkoani hapa baada ya kuvunjika mkono.
Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, na mwenyekiti mweza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), amevunjika mkono wa kushoto baada ya kuteleza na kuanguka.
Mmoja wa wasaidizi wake aliyejitambulisha kwa jina la Hamis, alisema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wakati akiondoka hotelini kurejea nyumbani kwake. Alisema Mbatia alikuwa akishuka ngazi katika Hoteli ya Uhuru iliyopo eneo la Shanty Town, ndipo alipoteleza na kuanguka.
“Tunamshukuru mungu kwa sasa anaendelea vinzuri na kwa bahati eneo alipoanguka kulikuwa na Daktari wa KCMC anaitwa Ansbert Swetbert ndiye alitoa huduma ya kwanza.
“DK. Ansbert alikuwa msaada mkubwa na ndiye alitusaidia na kumfikisha KCMC. Alikaa naye hadi saa nane usiku. Wauguzi na madaktari KCMC walimpa msaada mkubwa, kwa kweli tunamshukuru mungu,” alisema Hamis. Akizungumzia hali yake hospitalini hapo, Mbatia alisema bado maumivu aliyonayo ni makali kutokana na kuvunjika mkono.
“Bado ninamaumivu makali. Nashukuru sana mungu na jopo la madaktari limeshakutana na watafanya uamuzi,” alisema.
Alisema ameshapatiwa matibabu ya mwanzo baada ya vipimo vya X Ray kuthibitisha amevunjiaka mkono na kwamba madaktari wanafanya tathmini ni huduma gani zaidi apewe.
Comments