top of page

WADAU SERIKALINI WAKISHIRIKIANA UKATILI WA KIJINSIA UTAISHA

  • Khalidi
  • Dec 20, 2017
  • 2 min read

Maafisa ustawi wa jamii wanatakiwa kuhakikisha wanashirikiana na Jeshi la polisi pamoja na wananchi ili kuweka mipango dhabiti ya kuondoa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii. Hilo ni agizo la Mkuu wa Wilaya ya Ubongo, Kisari Makori, kwa watendaji hao kutokana na vitendo vya ukatili kuendelea kushamiri nchini.

Wiki iliyopita mtandao wa kijinsia Tanzania (TGNP) uliazimisha kampeni ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia. Maadhimisho hayo yalianza Novemba 25 na kuhitimishwa Desemba 10 mwaka huu, ambapo Makori alisema kutokana na vitendo hivyo kuendelea wananchi na wadau mbalimbali wanapaswa kushirikiana na serikali katika kutokomeza tatizo hilo.

Ripoti ya shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya mwaka 2015 inaonesha wanawake wanne kati ya kumi wamewahi kufanyiwa ukatili wa kijinsia.

“Ripoti inaonyesha asilimia 40 ya wanawake ambao wamewahi kuolewa wamefanyiwa ukatili na wenza wao ama ni wakingono au wa kimwili hiyo inaonyesha ni jinsi gani suala hili lilivyo kubwa. “Hivyo basi maafisa ustawi wa jamii wanatakiwa kuweka mipango thabiti ya kuhakikisha wanashirikiana na Jeshi la polisi na wananchi kuondoa vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii zetu,” alisema Makori.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Grace Kishetu, alisema maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ya ‘Funguka! Ukatili dhidi ya wanawake na watoto haumwachi mtu salama’ yamejikita katika kusisitiza moja ya kanuni za ajenda ya dunia ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu.

“Kampeni imelenga kupinga ukatili dhidi ya watoto kwa kuboresha mazingira yatakayo mwezesha mtoto wa kike kupata elimu sawa na wakiume na asilimia 72 ya wasichana wanakabiliwa na ukatili wa kimwili na kihisia,” alisema Grace.

Kama ambavyo takwimu mbalimbali zinaonyesha ukatili unaathari kubwa katika uchumi wan chi na maendeleo na inakadiriwa uzalishaji katika pato la Taifa unapotea kwa asilimia 1.2 hivyo jamii, wadau na serikali zinapaswa kushirikiana kwa pamoja kuondoa tatizo hili.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page