top of page

SADIFA ATOKA KWA DHAMANA

  • Khalidi
  • Dec 20, 2017
  • 1 min read

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Dodoma, imemwachia kwa dhamana aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma Khamis (35), aliyekamatwa Desemba 11 mwaka huu kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wapigakura wa Mkutano Mkuu wa jumuiya hiyo.

Akisoma uamuzi mdogo wa shauri hilo jana, kuhusu dhamana, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Fovo, alisema kuwa vigezo ambavyo vilitolewa na waajili wa serikali havihusiani kwa namna yoyote kuvuruga uchaguzi na kuingilia upelelezi kama ambavyo walidai upande wa mashtaka.

Alisema kuwa mshtakiwa anaruhusiwa kudhaminiwa kwani ni haki yake kikatiba kutokana na kifungu namba 15 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Mazingira ya kesi hii na vigezo vilivyotolewa na wakili wa serikali ni tofauti kabisa, hivyo sijaona sababu ya kumnyima dhamana,” alisema Hakimu Fovo.

Alisema kifungu cha 15 kidogo (b) walichokitumia mawakili wa serikali kutopewa dhamana kwa mtuhumiwa, hakimzuii mtu yeyote kupewa dhamana, hivyo upande wa Jamuhuri sababu zao hazikuwa na mashiko.

Desemba 11, mwaka huu, Sadifa alifikishwa mahakamani hapo na Takukuru na kusomewa makosa mawili, la kwanza likiwa ni kudai kutoa rushwa ya vinywaji kwa wapigakura akiwa katika makazi yake kata ya Mnadani Mjini Dodoma kuwashawishi kumchagua aliyekuwa mgombea wa nafasi ya makamu mwenyekiti UVCCM, Rashidi Rashidi.

Kosa la pili anadaiwa kutoa nauli kwa wapiga kura kutoka Dodoma kwenda Kagera akiwa katika makazi yake, Kata ya Mnadani mjini Dodoma kuwashawishi kumchagua mgombea huyo.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page