SHEIKH PONDA AIBWAGA JAMHURI MAHAKAMANI
- Khalidi
- Dec 19, 2017
- 1 min read

Mahakama Kuu ya Tanzania imetupilia mbali maombi ya rufaa yaliyowasilishwa na upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiisilamu, Sheikh Issa Ponda.
Katika kesi hiyo, Jamhuri ilikata rufaa ya kupinga hukumu inayotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro ya kumuachia huru Sheikh huyo katika kesi iliyokuwa inamkabili ya kutoa matamshi ya uchochezi.
Akisoma uamuzi huo mahakamani hapo , Jaji wa mahakama Kuu, Edson Mkasimongwa, alisema kuwa mahakama imemwachia huru Sheikh Ponda kwasababu hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Morogoro haikukosea.
Alisema anaunga mkono uamuzi huo na kumwachia huru Sheikh Ponda kwasababu hawajakosea katika uamuzi wao katika kesi ya kutoa matamshi ya uchochezi.
“Ninakubaliana na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Morogoro, kwa sababu hawajakosea katika uamuzi wake, hivyo basin a mimi natupilia mbali rufaa iliyotolewa na upande wa Jamhuri katika kesi ya kutoa matamshi ya uchochezi,” alisema Mkasomongwa.
Jaji Mkasimongwa alisema kuwa upande wa Jamuhuri haukupaswa kumshtaki Sheikh Ponda kwa kosa lilelile la kuvunja amri ya mahakama ya Kisutu, bali walitakiwa kuwarudisha katika mahakama hiyo ili imchukulie hatua zaidi.
Sheikh Ponda akiwa katika mahakama ya Morogoro alipandishwa kizimbani na kudai kuwa Agosti 10, 2013 katika eneo la uwanja wa ndege, Manispaa ya Morogoro, aliwaambia waislamu wasikubali uundwaji wa kamata za ulinzi na usalama za misikirti kwa madai kuwa zimeundwa na baraza la Kiisilamu tanzania (bakwata) ambao ni vibaraka wa CCM na serikali.
Akizungumza nje ya mahakama hiyo, Juma Nassoro ambaye ni wakili wa Shekh Ponda, aliunga mkono hukumu hiyo na kudai kuwa mahakama imetenda haki kwa mteja wake.
Comments