top of page

KASORO KUZUIA VIGODORO USIKU

  • Khalidi
  • Dec 18, 2017
  • 2 min read

Ngoma za asili, ikiwemo vigodoro, zinazopigwa nyakati za usiku na kuwashilikisha watoto wa kike imesadikika kuwa ndio chanzo kikubwa kinachoplekea mabinti kupata mimba za utotoni.

Akizindua maadhimisho ya mapambano dhidi ya ndoa za utotoni. Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe ambaye anakaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe alisema ngoma za asili zinazopigwa usiku zimechangia watoto wa kike kupata mimba kutokana na mazingira ya tamaduni hizo.

“Natoa agizo kwa ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya, Afisa Utamaduni kwa yeyote atakayekuja kutaka kibali kuhusu sherehe zozote nyingine za asili ambazo zitapigwa usiku, vibali vitakapotoka visishirikishe watoto katika sherehe hizo,” alisema Gondwe.

“Hatuwazuii kufanya tamaduni zenu lakini zifuate umri.”

Aidha Gondwe alitoa agizo kwa jeshi la polisi wilayani korogwe kufanya doria za mchana katika vibanda vya kuonyeshea picha ili kubaini maudhui yanayoonyeshwa kama yanafaa kuangaliwa na watoto na ikibaini ni kinyume, vibanda hivyo vifungiwe. “Hivi vibanda vya kuonyesha picha maarufu kama vibanda umiza tunajua watoto hawaruhusiwi kukaa zaidi ya saa 12 jioni, hivyo basi ikigundulika wahusika wanaonyesha picha mbaya kwa watoto au watoto kukaa mpaka usiku, biashara hizo zife.” Alisisitiza.

Gondwe pia aliwataka wadau wa elimu wakiwemo wazazi na walezi, kuacha kubweteka katika mapambano dhidi ya mimba na ndoa za utotoni kwa kuona idadi ya wanafunzi wanaopata mimba mashuleni ni ndogo ikilinganishwa na wilaya nyingine za mkoa wa Tanga.

Alisema takwimu kutoka idara ya elimu zinaonyesha mwaka 2016 watoto waliopata mimba mashuleni ni 11 kwa sekondari na msingi, na mwaka 2017 ni watoto 42.

“Kila mtoto lazima asome, mheshimiwa Rais(John Magufuli) ametoa fursa ya elimu bure kwa watoto wote kwahiyo hapa cha kufanya ni kuondoa kabisa tatizo la mimba,” alisema kaimu mkuu wa wilaya hiyo.

“Niseme tu kilashule iwe ya msingi au sekondari, kila mwalimu apewe watoto wa kuwasimamia na kuwashauri ili wawe huru kujieleza mambo yanayowaathiri katika masomo na maisha yao ya kila siku.”

Comentários


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page