SPIKA NDUGAI AELEZA SABABU ZA KUTOMTEMBELEA TUNDU LISSU
- David
- Dec 16, 2017
- 1 min read

Baada ya Mbunge wa Singida Mashariki kumlalamikia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai (Mb) kushindwa kwenda kumjulia hali, Spika amesema kuwa, kukosekana kwa hali ya utulivu nchini Kenya baada ya kufanyika uchaguzi, kulimfanya ashindwe kumtembelea Mbunge Tundu Lissu anayepatiwa matibabu katika Hospitali ya Nairobi.
Ndugai aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Kisasa mjini Dodoma na kueleza kwamba, yeye hawezi kwenda Dodoma kama ambavyo watu wengi wanakwenda na kutoka watakavyo.
Spika alisema kwamba, wabunge wanaweza kuingia Kenya na kumuona Lissu watakavyo, lakini kwake yeye ni vigumu.
“Ninapokwenda kule lazima kuwe na taarifa rasmi za kiserikali na za kibunge na ninapokelewa kihivyo. Na ninapopelekwa huko hospitali ama wapi napelekwa kwa namna hiyo ndio utaratibu wa nchi kwa nchi,” alisema Ndugai.
Ndugai ameongeza kuwa, kutokana na hali ilivyokuwa, haukuwa wakati mzuri yeye kwenda kwa sababu lingeweza kuzuka jambo lolote kwamba amekwenda na ajenda inayohusu masuala ya uchaguzi wa Kenya.
Baada ya sasa hali kuwa shwari, Spika alisema kwamba baada ya kumalizika kwa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya basi atakwenda kumuona Lissu kwa sababu bado ni mbunge halali wa Tanzania.
“Ni mbunge wetu, tunampenda na tuko naye na tusingependa asikitike kwa lolote lile,”alisema Ndugai huku akiongezea kwamba, tayari alikwishawatuma wabunge wawili ambao ni Mary Chatanda (Korogwe Mjini –CCM) na Faharia Khamis Shomari (Viti Maalumu-CCM) kwa niaba ya Bunge kwenda kumuona Lissu.
Lissu amelazwa katika Hospitali ya Nairobi akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi akiwa mjini Dodoma Septemba 7 mwaka huu.
Commentaires