top of page

IGP SIRRO AWAONYA WANAOHIFADHI WAKIMBIZI

  • Khalidi
  • Dec 15, 2017
  • 1 min read

Mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP), Simon Sirro, amewataka wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuacha tabia ya kuwapa hifadhi raia kutoka nchi jirani.

Sirro aliyasema hayo , wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma, baada ya kikao cha ulinzi na usalama cha Mkoa wa Kigoma. Alisema kwamba, wananchi wa Kigoma wengi wao wana tabia ya kupokea wakimbizi na kuwapa hifadhi kama ndugu zao na baadaye wakimbizi hao hushiriki katika matukio mbalimbali ya uhalifu, yakiwamo ya kutumia silaha.

“Changamoto ya kuhifadhi raia kutoka nchi jirani za Burundi na Congo isifumbiwe macho, kwa kuwa inachangia ongezeko la matukio ya kihalifu mkoani hapa Kigoma.

“Katika hili, ni lazima wananchi watambue kuwa, kitendo cha kupokea na kuhifadhi wahamiaji haramu, ikiwa ni pamoja na kuwapa kazi kama vibarua vya kulima, ni kosa kisheria na yeyote atakayekamatwa anahifadhi wahamiaji hao hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Kwa hiyo, nawataka wananchi wa Kigoma waache kuwahifadhi watu na badala yake wajenge tabia ya kutoa taarifa kwa vyombo husika kila wanapowaona wahamiaji haramu hao.

“Pamoja na hayo, nafurahi kusema kwamba , matukio ya uhalifu katika Mkoa wa Kigoma yamepungua, hasa matukio ya uporaji wa kutumia silaha, kwa sababu silaha nyingi zimekuwa zikikamatwa,” alisema IGP Sirro.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page