WAZIRI AFUNGA MGODI WA DHAHABU
- Khalidi
- Dec 14, 2017
- 1 min read

Serikali imefunga mgodi mdogo wa dhahabu ulioko kijiji cha Bulamba Wilaya ya Bunda mkoani Mara kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo tuhuma ya uharibifu wa mazingira.
Uharibifu huo umekuwa ukisababisha wakazi wa maeneo jirani kuathirika kiafya.
Serikali pia imeliagiza baraza la Taifa la usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha sheria ya mazingira inazingatiwa na wawekezaji wa migodi nchini.
Mgodi huo unaomilikiwa na Abdulazizi Hagebu, ulifungwa juzi na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola, baada ya kuutembelea kufuatia malalamiko kutoka kwa wananchi wa kijiji hicho kuhusu uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na mgodi huo, hivyo kuhatarisha afya zao.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho akiwamo Diwani wa kata hiyo, Abiud Chacha, walitoa kero hiyo kwa Naibu Waziri katika eneo la mgodi, huku wakidai mwekezaji amekuwa akiwatishia kuwakamata kwa kutumia polisi.
“Huyu bwana kwanza alitudanganya atatujengea kituo cha afya, nyumba ya mwalimu na darasa, lakini tunapokuwa tunamfuatilia na kukerwa na uharibifu huu wa mazingira amekuwa akitutishia kutukamata akiwamo hata mimi diwani,” alisema Chacha.
“Tunamdai kiasi cha sh milioni 6.5 kuazia mwaka 2005, lakini hadi leo hajatulipa, na baada ya kumfuatilia sana ndipo akatuwekea kwenye akaundi yetu sh. Milioni 1.8 tu. Hatumtaki kabisa,” alisema Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Daniel Kusoya.
Walisema pamoja na mwekezaji huyo kuchukua eneo hilo kwaajili ya uchimbaji wa dhahabu, baadaye alijimilikisha eneo kubwa zaidi yakiwamo mashamba yao na alifanya kwaajili ya kilimo cha pamba.
Na kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri alisema serikali ya Rais John Magufuli, ambayo ni ya mtetezi wa wanyonge haiwezi kukubali hali hiyo kuendelea na kutoa maagizo kadhaa, ikiwamo la kufunga mgodi huo, mpaka mwekezaji huyo atakapotimiza vigezo vyote vinavyotakiwa.
Comments